rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Israeli Palestina Benjamin Netanyahu

Imechapishwa • Imehaririwa

Machafuko Gaza: Israel yapinga uchunguzi wowote huru

media
Benjamin Netanyahu amefutilia mbali kauli za kuiokosoa Israel baada ya vurugu kwenye mpaka wa Gaza na Israeli siku ya Ijumaa (Machi 30). REUTERS/Ronen Zvulun

Siku mbili baada ya machafuko kwenye mpaka wa Gaza (Palestina) na Israeli yaliogharimu maisha ya Wapalestina 16, serikali ya Israel imekataa uchunguzi wowote huru wa kimataifa.


Baada ya makabiliano makali siku ya Ijumaa kati ya askari wa Israel na waandamanaji wa Palestina, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa mambo ya nje wa Ulaya Federica Mogherini wameomba kufanyike "uchunguzi huru" kuhusu matumizi ya risasi kwa upande wa jeshi la Israel. Ombi ambalo serikali ya Kiyahudi imekata kutii.

"Hatutashirikiana na tume yoyote ya uchunguzi," Waziri wa Ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman ameonya. "Wale ambao wanaomba uchunguzi ni wanafiki," ameongeza.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefutilia mbali kauli zinazoendelea kuikosoa nchi yake, ikiwa ni pamoja na kauli ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye ameishtumu Israel kufanya mashambulizi ya kikatili. "Hatupokei somo la kimaadili kutoka kwa mtu ambaye anaendelea kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia kwa miaka mingi," Bw Netanyahu alijibu kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Jeshi la Israel linakanusha kuwa Wapalestina 758 walijeruhiwa kwa risasi,amearifu mwandishi wetu mjini Jerusalem, Paulo Michel. Msemaji wa jeshi ameeleza kwamba Wapalestina kumi waliouawa walishiriki katika siku za nyuma katika "shughuli za kigaidi" katika kundi la Hamas na katika makundi mengine ya wapiganaji katika Ukanda wa Gaza.

Ufaransa inaomba pande zote "kujizuia"

Siku ya Jumapili Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa (Quai d'Orsay) ilielezea wasi wasi wake kufuatia machafuko ya siku za hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza" na kutoa wito kwa serikali ya Israel kujizuia".

"Ufaransa inakumbusha mamlaka ya Israel wajibu wake wa kulinda raia na kuiomba kujizuia," taarifa kutoka Wizara ya ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilisema.