Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA-ELIMU-UWEKEZAJI

Ufaransa: Tunaunga mkono 100% juhudi za Tanzania kufikia uchumi wa kati

Serikali ya Ufaransa imesema inaunga mkono kwa asilimia 100 juhudi za rais wa Tanzania John Pombe Magufuli katika kuijenga Tanzania mpya na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Balozi Clavier akizungumzia siku ya Kitaifa ya Ufaransa mwaka huu
Balozi Clavier akizungumzia siku ya Kitaifa ya Ufaransa mwaka huu Picha;Venance Nestory
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza jijini Dar Es Salaam kuelekea maadhimisho ya sherehe za kitaifa za Ufaransa “Bastille Day”, balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Frederic Clavier, amesema nchi yake inaridhishwa na kasi ambayo Tanzania inaenda nayo katika kufikia lengo hili.

Balozi Clavier amesema katika kuunga mkono juhudi hizo za Serikali, Ufaransa imeendelea kutoa mikopo nafuu na msaada wa kifedha kupitia shirika lake la maendeleo AFD.

Amesema katika kuona hilo, ameielekeza AFD kutoa ufadhili wa kutosha kwenye miradi muhimu ya Serikali kama vile ile ya nishati, usafiri na maji.

Balozi Clavier ameongeza kuwa kupitia ufadhili wa shirika la maendeleo ya Ufaransa, limeongeza kwa zaidi ya mara mbili mikopo yake kwa Serikali hadi kufikia dola za Marekani milioni 110 na fedha za msaada kufikia dola za Marekani milioni 23.

“Kutokana na urafiki wa muda mrefu kati ya nchi zetu mbili, Ufaransa imeendelea kusaidia pakubwa kwenye sekta ya afya na ndio maana tumetoa kiasi cha dola milioni 53 kama mkopo kusaidia upanuzi wa hospitali ya Agha Khan”, alisema balozi Clavier.

Mbali na kwenye sekta ya afya, balozi Clavier amesema Ufaransa imeendelea kushawishi makampuni ya Kifaransa kuwekeza nchini Tanzania, akitolea mfano uwepo wa makampuni zaidi ya 50 ya Kifaransa yaliyowekeza kwenye kilimo na nishati.

“Kutokana na umuhimu wa kilimo kwa nchi ya Tanzania, Ufaransa imetoa kiasi cha dola milioni 1 kuwasaidia wakulima wadogo kwenye mkoa wa Mtwara pamoja ujenzi wa kiwanda cha mihogo mkoani Lindi ambacho kimetengeneza ajira 470 kwa watanzania,” alisema balozi.

Balozi Clavier ameongeza kuwa kwa sasa nchi ya Tanzania na Ufaransa zinafanya biashara zaidi kuliko awali ambapo kwa mwaka 2018 ufanyaji biashara umeongezeka kwa asilimia 30 zilizofikia thamani ya dola za Marekani milioni 200.

Akigusia kuhusu ushirikiano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Ufaransa, balozi Clavier amesema tayari kuna mpango na mchakato umeshakamilika wa kuanzisha shirikisho la wafanyabiashara wa Ufaransa na Tanzania, jukwaaambalo amesema litasaidia kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili.

“Tunatarajia uundwaji wa chombo hiki kukamilika ndani ya miezi michache ijayo, ambapo makampuni 40 ya Ufaransa yanayofanya shughuli zake nchini Tanzania yatakuwa wanachama lakini tunakaribisha makampuni yote ya Tanzania kuwa wanachama hatua itakayowezesha yafanye biashara nchini Ufaransa,” alisema balozi Clavier.

Kuhusu sekta ya Elimu, balozi Clavier amesema nchi yake imeendelea kuwa mshirika wa karibu wa wizara ya elimu, ambapo katika kuonesha ushirikiano thabiti uliopo, Ufaransa imefungua shule ya Kifaransa iliyoko masaki ambapo wageni na raia wa Tanzania wanayofursa ya kusoma hapo.

Balozi Clavier ameongeza mbali na shule ya Kifaransa, wamefungua fursa kwa wanafunzi nchini Tanzania kwenda kusoma Ufaransa, ambapo wamefungua vituo vya taarifa kuhusu vyuo vikuu vya Ufaransa katika chuo kikuu cha Dar es Salaam na DUCE.

Amesema lengo la vituo hivi ni kutoa nafasi ya wanafunzi kufahamu vyuo vilivyoko Ufaransa na kozi ambazo wanaweza kwenda kusoma na kwamba wameenda mbali zaidi kuanzisha jukwaa la wanafunzi wa Tanzania waliosoma Ufaransa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.