Pata taarifa kuu
RWANDA-KIMBARI-1994-AMANI

Wanyarwanda waadhimisha miaka 25 baada ya kutokea kwa mauaji ya kimbari

Rwanda inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 25, tangu kutokea kwa mauaji mabaya ya kimbari yaliyosababisha vifo vya watu 800,000 wengi wao wakiwa Watutsi.

Eneo la kumbukumbu la mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994
Eneo la kumbukumbu la mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 Jacques NKINZINGABO / AFP
Matangazo ya kibiashara

Mauaji hayo ya mwaka 1994, yalichukua karibu siku 100 kabla ya kusitishwa na yanasalia kuwa mabaya zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Rais Paul Kagame, anawaongoza  wananchi wa taifa hilo, kukumbuka wale wote waliopoteza maisha wakiwemo watoto zaidi ya 300, 000 kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Imekuwa ni wiki inayofahamika kama Kwibuka, kuwakumbuka wote walioangamia, huku raia wa nchi hiyo wakiapa kuwa kilichotokea, hakitatokea tena.

Baadhi ya raia wa nchi hiyo waliokuwa wadogo wakati huo, wengi hao hawafahamu wapendwa wao walizikwa wapi na imekuwa ni wiki ngumu kwao kukumbuka kilichotokea.

Machafuko yalizuka Aprili tarehe 6 mwaka 1994, baada ya ndege iliyokuwa imembeba rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote wakiwa wa Kabila la Hutu, kuangushwa.

Muda mfupi baada ya ajali hiyo, walinzi wa rais walianza kuwauwa Watutsi.

Kundi la waasi la Rwandan Patriotic Front (RPF), ambalo lilikuwa na Watutsi wengi, waliwashtumu Wahutu wenye msimamo mkali ndani ya serikali kuiangusha ndege hiyo, huku serikali ikishtumu waasi wa RPF kuhusika.

Hadi sasa haijafahamika vema ni nani aliyehusika na tukio la kuiangusha ndege hiyo.

Hata hivyo, nchi ya Rwanda, imekuwa ikiishtumu Ufaransa kwa kuhusika pakubwa katika upangaji wa mauaji hayo, madai ambayo imeendelea kukanusha.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.