Pata taarifa kuu
SUDANI KUSINI-UNHCR-EBOLA-AFYA

UNHCR: Sudan Kusini inaweza kukabiliwa na ugonjwa hatari wa Ebola

Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia wakimbizi UNHCR, inahofia kuwa huenda ugonjwa hatari wa Ebola ukaingia nchini Sudan Kusini, kwa sababu ya ongezeko la wakimbizi kutoka DRC.

Maafisa wa Afya wakiendelea na shughuli zao za kuzuia na kupambana dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola , mashariki mwa DRC.
Maafisa wa Afya wakiendelea na shughuli zao za kuzuia na kupambana dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola , mashariki mwa DRC. Luis Encinas/MSF
Matangazo ya kibiashara

Jimbo ambalo lipo hatarini ni lile la Yei, ambalo limeendelea kupokea wakimbizi kutoka nchi jirani na wiki hii, wakimbizi 42 wametoka DRC.

UNHCR imeamua kutoa elimu kwa raia wa Jimbo la Yei, kufahamu namna ya kutambua na kujikinga na ugonjwa huo hatari.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya tarehe 5 Novemba 2018, idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia ugonjwa wa Ebola imefikia 189.

Mapema wiki hii wizara ya afya nchini Uganda ilitangaza kwamba imeanza kutoa chanjo ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola nchini humo licha ya kutoripotiwa kwa maambukizi yoyote.

Chanjo hiyo ilianza kutolewa kwa wafanyakazi wa afya, kuanzia siku ya Jumatatu, kama tahadhari kwa sababu ya kuendelea kusambaa kwa ugonjwa huo Mashariki mwa DRC, katika Wilaya ya Beni inayopakana na Uganda.

Mapema juma lililopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kauli moja azimio linalotaka kuimarisha uwezo zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola mashariki mwa DRC.

Wanadiplomasia wametoa wito kwa makundi yote ya waasi, na hasa kundi la waasi wa Uganda la Allied Democratic Forces (ADF), kusitisha shughuli zao ili kuwezesha haraka utoaji wa misaada na usiozuilika. Wataalamu wa masuala ya afya wana hofu kuwa kukosekana kwa huduma za afya, janga hilo linaweza kusambaa hadi katika nchi nyingine za ukanda huo kama vile Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.