rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Tanzania

Imechapishwa • Imehaririwa

Operesheni ya kumtafuta Mohamed Dewji yaendelea Tanzania

media
Mohammed Dewji akifanya mazoezi na mwanae. Mohammed dewji/twitter.com

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama nchini Tanzania vinaendelea na jitihada za kumtafuta Mfanyabiashara Mohamed Dewji maarufu kwa jina la Mo aliyetekwa na watu wasiofahamika.


Kuna taarifa ambazo zinaendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Tanzania kwamba Mohamed Dewji amepatikana, lakini Kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema Mo Dewji kufikia sasa bado hajapatikana.

“Dewji bado tunaendelea kumfuatilia na kuwafuatilia watu waliofanya uhalifu huo, wa kumteka.

“Zipo taarifa mtaani kwamba ameshapatikana, wengine wanadai kwamba amepatikana kule Coco Beach lakini taarifa kutoka meza yangu hii, na taarifa ambazo sasa ni taarifa rasmi, bado hajapatikana wala wahusika bado hawajakamatwa.

Dewji ni tajiri kijana barani Afrika ambaye mbali na kumiliki kampuni mbalimbali chini ya kampuni mama ya Mohammed Entreprises Tanzanial Limited (MeTL), pia ni mwekezaji katika klabu maarufu nchini humo ya Simba, anamiliki asilimia 49 ya hisa.

Ripoti za mapema zimearifu kwamba Dewji 43 alitekwa katika hoteli moja Jijini Dar es Salaam alikofika kwa ajili ya mazoezi hapo siku ya Alhamisi wiki hii.Taarifa za awali zinazonesha waliohusika katika utekaji wa mfanyabiashara huyo ni watu wawili ambao ni raia wa kigeni.

Lakini Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema watuhumiwa wanaoshikiliwa kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara Mo Dewji wamefikia 12.