Pata taarifa kuu
TANZANIA-TASNIA

Muigizaji mkongwe Mzee Majuto afariki dunia

Msanii mkongwe wa vichekesho Amri Athuman maarufu King Majuto, amefariki dunia usiku Jumatano kuamkia Alhamisi wiki hii baada ya kulazwa siku chache zilizopita katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli akimjulia hali Mzee Majuto katika Hospitali ya Muhimbili.
Rais Magufuli akimjulia hali Mzee Majuto katika Hospitali ya Muhimbili. Ikulu, Tanzania
Matangazo ya kibiashara

Taarifa za msiba huo wa nguli wa maigizo zimethibitishwa na Afisa habari wa Muhimbili Aminiel Eligaisha ambapo amesema Mzee Majuto amefariki akiwa anaendelea na matibabu ambayo aliyaanza Julai 31, mwaka huu baada ya jitihada za madaktari kuokoa uhai wake kushindikana.

''Hali yake ilibadilika majira ya saa tisa alasiri ya leo hivyo kuhamishwa kutoka jengo la Sewahaji kwenda ICU. Ilipofika saa 1.30 jioni hii hali yake ilibadilika zaidi na madaktari walijitahidi kuokoa maisha yale bila mafanikio. Ilipofika saa mbili alikata roho'', amesema.

Moja ya Tamthilia alizocheza King Majuto ni Hii hapa:

Mzee Majuto alianza kuumwa muda mrefu akisumbuliwa na tatizo la nyonga ambapo mapema mwezi Mei alipelekwa nchini India kwaajili ya matibabu kabla ya kurejea nchini mwezi Juni ambapo alifikia Muhimbili lakini baadae alipata nafuu na kwenda nyumbani kabla ya kurudishwa tena Muhimbili baada ya hali yake kubadilika.

Mkongwe huyo alitangaza kustaafu kuigiza baada ya kutoka India lakini atakumbukwa kwa kazi zake nyingi za kuchekesha ambazo alizifanya kwa uhodari mkubwa na kuwavutiwa mashabiki wengi.

Mzee Majuto ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kwenye filamu alianza kuugua mwaka jana na mwaka huu serikali kwa kushirikana na wananchi walichanga pesa na kumpelekeka kwenye matibabu nchini India.

Muigizaji huyo alizaliwa mnamo mwaka 1948 jijini Tanga na kusoma shule Msambwini, Tanga, alianza kuigiza mnamo mwaka 1958 akiwa na umri wa miaka 9.

Marehemu Majuto alianza maisha kwa kujishughulisha na shughuli za kilimo kabla ya kuingia kwenye sanaa ya maigizo ambayo ilimpatia umaarufu.

Taarifa ya ikulu imesema King Majuto amefariki dunia majira ya saa 1:30 Jioni siku ya Jumatano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

Rais Magufuli amesema King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za chama na Serikali katika kuhimiza maendeleo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.