rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Kenya Uhuru Kenyatta Siasa

Imechapishwa • Imehaririwa

Ufisadi unavyowatesa Wakenya

media
Picha ya bendera ya Kenya youtube

Ufisadi ni hali ya kuamua kudanganya na kunuifaika kwa kutoa au kupokea mali kama fedha, kwa manufaa fulani.


Ni hali ambayo imeendelea kuyatesa mataifa mbalimbali duniani hasa barani Afrika, na kurudisha nyuma maendeleo.

Sheria zimetungwa kupambana na hali hii, kuna watu wameteuliwa kusaidia katika viti hivi, lakini mambo yameendelea kuwa magumu.

Ufisadi katika nchi ya Kenya, ni suala ambalo limewaacha Wakenya wengi na hasira kubwa kwa sababu fedha zao ndizo zinazoibiwa.

Hata hivyo, hili ni suala ambalo limekuwa likishuhudiwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki mwa miaka zaidi ya 50 sasa, tangu uhuru wa nchi hiyo chini ya rais wa kwanza Jomo Kenyatta.

Kashfa ya kwanza kuwahi kuripotiwa wakati wa rais wa kwanza wa nchi hiyo, ilikuwa ni mwaka 1965, wakati Waziri wa Biashara na Mashirika ya ya umma Paul Ngei, alipodaiwa kusababisha uhaba wa mahindi nchini humo.

Baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa, mke wa Waziri huyo Emma Ngei, alinunua mahindi moja kwa moja kutoka kwa wakulima na kuyahifadhi katika ghala yake kinyume na sheria wakati huo.

Ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme katika eneo la Tukwel ni kashfa nyingine kubwa ya ufisadi iliyowahi kuripotiwa nchini Kenya kati ya mwaka 1986 na 1991.

Ilidaiwa kuwa kiwango cha fedha kilichotengewa mradi huo, kilikuwa mara tatu zaidi ya bajeti iliyokuwa imekubaliwa na serikali. Hata baada ya ujenzi wa kituo hicho, kiwango chake kilikuwa cha chini.

Hata hivyo, kashfa kubwa ambayo imewahi kuripoti nchini humo ilikuwa ni ile ya Goldenberg iliyoanza kusumbua vichwa vya watu tangu miaka ya tisini.

Serikali ya Kenya iliingia katika mkataba wa kibiashara na kampuni ya Goldenberg International ili kujihusisha na biashara ya dhahabu, ilisababisha nchi hiyo kupoteza Mabilioni ya fedha na baada ya uchunguzi na hata baadhi ya viongozi wakuu serikali kushtakiwa, hakuna aliyefungwa jela.

Mbali na Goldenberg, wakati wa uongozi wa rais wa zamani Mwai Kibaki, nchi hiyo ilishuhudia kashafa nyingine ya kupotea kwa fedha za umma, iliyopewa jina la la Anglo leasing.

Hii ni kashfa ambayo serikali ya Kenya ilikuwa na mpango wa kubadilisha mfumo wake wa kutengeza pasi za kusafiria kwa kununua mitambo mpya.

Licha ya rais wa huo aliyekuwa ameapa kupambana na ufisadi, ilibainika baadaye kuwa badala ya mradi huo kutumia Euro Milioni 6, serikali ilitumia Euro Milioni 30.

Baada ya uchunguzi, Waziri wa Mambo ya ndani wakati huo, Christopher Murungaru na aliyekuwa Makamu wa rais Moody Awori, walitajwa lakini hakuna hatua iliychukuliwa dhidi yao. Waziri mwingine wakati huo Kiraitu Murungi ambaye kwa sasa ni Gavana alipinga kuhusika.

Wizi mkubwa wa fedha za umma ambao umefanyika wakati wa uongozi wa serikali ya sasa Uhuru Kenyatta, ni kupotea kwa Dola Milioni 80 katika Shirika la huduma kwa vijana NYS.

Watu 54 akiwamo Katibu Mkuu katika Wizara ya Vijana Bi.Lilian Ommolo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai wamekamatwa kwa madai ya kuhusika katika ufisadi huu, madai ambayo wamekanusha.

Imeripotiwa kuwa, Shirika hilo lilitumia Dola Milioni 10 kuwanunua nyama wanafunzi katika Shirika hilo, kwa kila mwaka, ikiwa na maana kuwa mwanafunzi mmoja alistahili kula nyama Kilo 66 kila siku.

Gurudumu moja la gari lilinunuliwa kwa Dola Milioni 1, huku wafanyikazi wengine wakilipwa fedha kwa kutofanya kazi yoyote.

Mbali na kashfa hii, imebainika kuwa Dola Milioni 30, zilitumiwa kuwalipa wafanyibiashara ghusi waliowauzia mahindi serikali, huku wakulima halisi wakiachwa.

Shirika la Kimataifa la kupambana na ufisadi Transparency International, imeiorodhesha Kenya katika nafasi ya 143 kati ya mataifa 180 duniani.

Profesa wa sheria PLO Lumumba, raia wa Kenya ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kukemea ufisadi na kutoa mihadhara ya namna ya kukabiliana na hali, hii amekuwa akisema chanzo kikubwa cha ufisadi ni uongozi mbaya.

Mwanaharakati wa kupambana na rushwa nchini Kenya Andrew Okoite Omtata ameimbia RFI Kiswahili, kwamba tuhuma za rushwa si ngeni katika taifa hilo.

"Mara zote wanaokamatwa ni maofisa  wa chini lakini hawa sio wanaofanya uamuzi, mawaziri na maofisa wengine wa ngazi za juu pia wanapaswa kuwajibishwa,"

Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akisema, amefanya vya kutosha kupambana na ufisadi na watu wanaomuangusha ni idara husika, kama Tume ya kupambana na ufisadi, Idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai, Ofisi ya mashtaka ya umma na idara ya Mahakama.

“Mnataka nifanye nini,” hii ni mojawapo ya kauli ya rais Kenyatta alipowahi kuulizwa kuhusu juhudi anazofanya kupambana na ufisadi katika nchi yake.

Chanzo kingine cha ufisadi, ni taasisi ambazo hazifanyi kazi yao ipasavyo hasa upande wa kiongozi wa Mashtaka kuwasilisha ushahidi wa kutosha Mahakamani, ili washukiwa wachukuliwe hatua.

Katika historia ya vita dhidi ya ufisadi, Majaji nchini Kenya pia wamewahi kushtumiwa kupokea rushwa na hivyo kukatisha matumaini ya kupatikana kwa haki.

Profesa PLO Lumumba katika mihadhara yake pia amekuwa akisisitiza kuwa, ni lazima wananchi wa kawaida kubadilisha mitazamo yao kuhusu ufisadi na kuacha tabia za kutoa fedha ili kusaidiwa kupata huduma fulani.

Pamoja na hilo, katika vita hivi, ni muhimu sana kwa wale wote wanaoongoza na washukiwa, kuchunguzwa na kufanyiwa udadisi ili kufahamika ni vipi walipata mali zao.

Mafanikio ya ufisadi yanaweza kuonekana iwapo kila mmoja atashiriki kikamifu katika nafasi yake, na kusaidia kuimarika kwa uchumi, utakaosaidia kupambana na ukosefu wa kazi na umasikini.

Wanaoendelea kuteseka kwa wizi wa fedha za umma ni wananchi wenyewe.

Licha ya hatua iliyochukuliwa hadi sasa na serikali, wengi hawana imani kuwa waliotajwa watachukuliwa hatua yoyote kwa sababu ya historia ya kesi za ufisadi nchini humo kwa sababu wana fedha za kuwarubuni viongozi wa taasisi mbalimbali.