rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Kenya Uhuru Kenyatta Siasa

Imechapishwa • Imehaririwa

Washukiwa wa ufisadi wakamatwa nchini Kenya

media
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la huduma kwa Vijana nchini Kenya NYS, Richard Ndubai aliyekamatwa Mei 28 2018 twitter.com/DG_Ndubai

Maafisa wanne wa nyadhifa za juu kutoka Shirika la huduma kwa vijana nchini Kenya NYS, wamekamatwa wakihusishwa na kashfa ya ufisadi katika Shirika hilo ambalo limepoteza Mabilioni ya fedha za nchi hiyo.


Baada ya thathmini iliyofanywa na mkaguzi wa serikali nchini humo, imebainika kuwa Shilingi Bilioni 9 zilipotea huku watu wakilipwa fedha kwa huduma ambazo hawakuzitoa.

Hatua hii imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji kupokea faili 10 za washukiwa mbalimbali na kuagiza wakamatwe na kufikishwa Mahakamani.

Miongoni mwa wale waliokamatwa ni pamoja na Richard Ndubai, Mkurugenzi Mkuu wa NYS, pamoja na msaidizi wake Sam Michuki.

Wengine ni Mkuu wa kitengo cha fedha, huku mshukiwa wa nne, akiwa hafahamiki.

Naye, Katibu Mkuu katika Wizara ya Vijana Lilian Mbogo Omollo amejisalimisha katika kituo cha Polisi baada ya kudaiwa kuhusika katika kashfa hiyo.

Wiki iliyopita, Bi.Omollo alikanusha madai ya fedha hizo kutoweka alipokuwa anahojiwa na wabunge na kueleza kuwa kama ingekuwa kweli, Shirika hilo lingekuwa limefungwa.

Hii ni mara ya kwanza, kwa maafisa wa juu wa serikali ya Kenya kukamatwa kwa madai ya ufisadi, baada ya shinikizo kutoka kwa raia wa nchi hiyo kupitia mitandao ya kijamii.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye anaongoza nchi hiyo, kwa muhula wake wa mwisho, ametaka washukiwa wote kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.