UNSC yatangaza vikwazo dhidi ya waziri wa ulinzi wa Sudan Kusini
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limemwekea vikwazo Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini Kuol Manyang Juk. Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imetangaza kuwa inaunga mkono hatua hiyo.
Imechapishwa:
Hatua hii imechukuliwa kwa kile kinachoelezwa kuwa Bwana Juk amendelea kusababisha mapigano kuendelea nchini humo.
Baraza hilo linasema, mwaka 2017, Waziri huyo aliwapa silaha wapiganaji wa SPLM-N kushambulia makao makuu ya wapiganaji wa upinzani katika eneo la Pagak.
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD hivi karibuni ilitangaza kuwa inaunga mkono hatua ya kuwekewa vikwazo viongozi na shakhsia wote wanaokwamisha jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro nchini Sudan Kusini.
Sudan Kusini, ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.
Umoja wa Mataifa umeendelea kuonya kuwa yeyote, anayeendelea kusababisha mapigano nchini Sudan Kusini, atawekewa vikwazo.
Machafuko nchini Sudan Kusini yamesababisha vifo maelfu ya watu na wengine mamilioni kuyahama makazi yao.