rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Kenya Uhuru Kenyatta Raila Odinga

Imechapishwa • Imehaririwa

Kenyatta: Naomba tuungane pamoja na Raila Odinga kuhubiri maridhiano

media
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anasema hatua yake ya kumaliza tofauti zake za kisiasa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ilikuwa ni kwa sababu ya Umoja wa taifa la Kenya. REUTERS/Thomas Mukoya

Rais Uhuru Kenyatta amelihotubia bunge, ikiwa ni hotuba yake ya kwanza tangu kuapishwa kuongoza muhula wa mwisho baada ya uchaguzi ulioligawa taifa hilo mwaka uliopita.


Kenyatta amewaambia wabunge na maseneta kuungana naye pamoja na kiongozi wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga ili kuhubiri maridhiano baada ya Uchaguzi wa mwaka uliopita.

Aidha amesema mauaji na uharibifu wa mali uliojitokeza wakati wa Uchaguzi uliopita, haustahili kujitokeza tena katika historia ya nchi hiyo huku akiomba radhi kwa Wakenya iwapo matamshi aliyoyatoa wakati wa kipindi cha kisiasa kuwagawa wananchi wa taufa hilo.

"Naomba radhi iwapo maneno yangu, yaliwafanya wakenya kugawanyika, kipindi cha kisiasa," alisema Kenyatta.

Aidha, ameongeza kuwa hatua yake ya kumaliza tofauti zake za kisiasa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ilikuwa ni kwa sababu ya Umoja wa taifa hilo.

Kuhusu usalama, rais Kenyatta amesema nchi hiyo iko salama licha ya kuendelea kuwepo kwa magaidi wa Al Shabab katika nchi jirani ya Somalia.

Kenyatta ameongeza kuwa vyombo vya usalama vimeendelea kuwa imara kuhakikisha kuwa wananchi wa taifa hilo wanakuwa salama.

Kwa mara ya kwanza hotuba ya rais Kenyatta leo ilihudhuriwa na maseneta na wabunge wa upinzani baada ya mwafaka wa kisiasa mwezi Machi kati ya rais huyo na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, rais anahitajika kulihotubia bunge angalau mara moja kwa mwaka kuwaeleza Wakenya kuhusu mipango ya serikali yake.