Pata taarifa kuu
BURUNDI-HRW-HAKI

Polisi yaruhusiwa kufanya misako ya usiku bila kibali maalum Burundi

Wabunge nchini Burundi wamepitisha muswada unaowaruhusu Polisi kufanya msako usiku bila ya kuwa na kibali maalum. Maseneta nao wanatarajiwa kuujadili mswada huo na kuupigia kura kabla ya kutiwa saini na rais Pierre Nkurunziza.

Polisi ikipiga doria katika wilaya Ngagara, Bujumbura, Avril 25, 2015.
Polisi ikipiga doria katika wilaya Ngagara, Bujumbura, Avril 25, 2015. AFP PHOTO / SIMON MAINA
Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa marekebisho yaliyofanyiwa sheria hii ya jinahi nchini Burundi ni pamoja na kipengele kipya kinachoviruhusu vyombo vya usalama kufanya misako usiku bila hata kuhitaji kibali maalum kutoka kwa mwendesha mashitaka kama ilivyokuwa awali. Baadhi ya wabunge hasa wale wa upinzani wa muungano matumaini ya Warundi (FNL-UPRONA) unaoongozwa na Agathon Rwasa wamebaini wasiwasi wao.

“Mimi nina wasiwasi kwa sababu mambo ya usiku ni ya usiku, kuna watu wanaozingishiana. Naweza kuja kufanya msako kwako tukiwa na ugomvi fulani kisha nikakufanyia kibaya, “ mbunge mmoja kutoka muungano huo amesema.

“Msako wa usiku ni swala gumu sana. Mtu hatojuwa ni nani anayepiga hodi ili afungue mlango. Na isitoshe hii ni kinyume na usemi wa kila siku wa viongozi kwamba nchi ni shwari, nchi ikiwa shwari hakuna misako ya usiku ni mpaka asubuhi, “ mbunge mwengine kutoka muungano huo amesema.

Upande wake waziri wa Burundi wa sheria Aime-Laurentine Kanyana, bila ufafanuzi wa kina amesema kuwa utaratibu huu ni kwa ajili ya kupiga vita vitendo vya uhalifu vinavyoshuhudiwa nchini.

“Eti msako wa usiku unatia uoga wasubiri asubuhi? Hapa niseme, kwa kuwa tumeshaona kwamba kuna mambo yasiyo mazuri yanayotendeka, lazima sheria zetu tuziambatanishe na wakati ili kupiga vita mambo hayo. Sio hapa Burundi tu sheria kama hizi zipo hata katika nchi zingine na zinatumika< “ amesema Waziri Kanyana.

Mashirika yanayotetea haki za binadamu kutoka Burundi yaliyo ukimbizini na yale ya kimataifa yamekosoa vikali hatua hiyo ya wabunge yakibaini kwamba wabunge wamekua wakipigia kura miswaada isyo na ulazima kwa kuhofia usalama wao.

Hatua hii inakuja wakati huu nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na wasiwasi wa kisiasa na kuendelea kwa madai ya maafisa wa usalama kuwashambulia wapinzani wa serikali kuelekea kura ya maoni kubadilisha Katiba mwezi ujao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.