rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Kenya Uhuru Kenyatta

Imechapishwa • Imehaririwa

Wachambuzi: Uhuru wa habari mashakani Kenya

media
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta. REUTERS/Thomas Mukoya

Wachambuzi nane wanaofanya kazi na kituo kimoja kikubwa cha habari nchini Kenya wametangaza kuacha kazi yao katika kile walichokisema ni kuongezeka kwa vitendo vya Serikali kuingilia shughuli za vyombo vya habari na kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari.


Wachambuzi hao waliokuwa na kurasa kwenye magazeti ni pamoja na George Kegoro mkurugenzi wa tume ya haki za binadamu Kenya, Lynne Muthoni Wanyeki mkurugenzi wa Afrika wa taasisi ya mfuko wa Open Society na Nic Cheeseman mhadhiri wa masuala ya demokrasia katika chuo kikuu cha Birmingham nchini Uingereza.

“Najiuzulu kupinga kuongezeka kwa mbinyo wa uhuru wa vyombo vya habari. Najizulu kuonesha mshikamano na sauti ambazo zimenaymazishwa. Najiuzulu kwa sababu tunapaswa kuishi kwa imani zetu,” amesema Cheeseman kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter.

Katika taarifa yao ya pamoja, wanane hao wameainisha matukio kadhaa yaliyotokea kwenye miaka ya hivi karibuni, wakitolea mfano kuingiliwa kwa uhuru wa kampuni ya Nation Media Group NMG.

Hii ikiwemo kufutwa kazi kwa mhariri mtendaji baada ya kuchapisha habari iliyomkosoa rais Uhuru Kenyatta na kushindwa kumpa mkataba mwingine mchora katuni maarufu Gado ambaye alikuwa akiilenga Serikali.

Mwezi uliopita kampuni ya NMG ilimfuta kazi meneja wa NTV Linus Kaikai baada ya kusema kulikuwa na muingiliano kati ya wamili na Serikali katika kusimamia uripotiji wa sherehe za kuapishwa kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Kituo cha NTV na vituo vingine viwili vilizimwa kwa juma moja licha ya agizo la mahakama kuagiza vyombo hivyo kuwashwa tena wakati walipojaribu kuripoti kuapishwa kwa Odinga.

Kuzimwa kwa vyombo hivyo vya habari kulikashifiwa pia na umoja wa Mataifa, Marekani na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

“Kuna mambo yanaogopesha hasa kuona kuwa Serikali ina uwezo wa kusema nani afanye kazi na nani asifanye kazi na kampuni ya NMG.

Kampuni ya NMG ni moja ya kampuni kubwa zaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ikifanya kazi nchini Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda.