Pata taarifa kuu
TANZANIA-ELIMU

Mkapa: Tanzania inahitaji mjadala wa kitaifa kuhusu elimu

Rais mstaafu wa awamu ya tatu nchini Tanzania Benjamin Mkapa ametoa wito wa kufanyika kwa majadilinao ya kitaifa kuhusu mwenendo wa sekta ya elimu nchini humo.

Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa. UN Photo/JC McIlwaine
Matangazo ya kibiashara

Mkapa ambaye ni mkuu wa chuo kikuu cha Dodoma nchini Tanzania, amesema hayo hapo jana wakati wa shughuli za kumuingiza kazini mkuu mpya wa chuo hicho.

Kwenye hotuba yake rais Mkapa amesema anashangazwa na matokeo mabaya ambayo yanashuhudiwa kila mwaka kutoka kwa shule za Serikali ukilinganisha na shule binafsi.

Mkapa amesema wakati umefika sasa wa mfumo wa elimu kutazamwa upya ikiwa ni pamoja na kuangalia changamoto zinazoikabili sketa hiyo ili kubaini wapi kuna dosari katika kuboresha elimu inayotolewa kwa shule za Serikali.

"Naambiwa kuwa elimu yetu ndio iko chini zaidi katika nchi wanachama za jumuiya ya Afrika Mashariki, sina hakika kwa kuwa sifahamu, hata hivyo ni muhimu kuwa na mjadala wa kitaifa ambao utakuwa shirikishi bila kujali kada ya raia." alisema Mkapa.

Rais huyo mstaafu ameongeza kuwa huwa anajiuliza ni kwanini kila matokeo yanapotangazwa na baraza la mitihani, kati ya shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa haukosi shule 8 za binafsi na labda shule mbili zinaweza kuwa za Serikali.

"Hapa kuna tatizo lazima tuuangalie upya mfumo wetu wa elimu ili uendane na mahitaji ya sasa." aliongeza Mkapa.

"Najua kuna watu watasema nalalamika sana, lakini hapana na mimi ni mwananchi wa kawaida," alieleza.

Licha ya juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuboresha mfumo wa elimu nchini humo ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu bure kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi Sekondari, bado inakabiliwa na changamoto ikiwemo miundombinu kama vile mishahara ya walimu, vifaa vya kufundishia na majengo ya shule.

Kupitia mpango wa kitaofa wa matokeo makubwa sasa nchi ya Tanzania imefanikiwa pakubwa katika ujenzi wa shule za kata katika kila wilaya pamoja na kuhamaisha wananchi kuchangia madawati na ujenzi wa nyumba za walimu.

Hata hivyo shule za Serikali zimekuwa hazifanyi vizuri katika mitihani ya kitaifa ukilinganisha na shule binafsi ambazo mara nyingi zimekuwa zikiongoza katika matokeo ya mitihani ya taifa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.