rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Kenya Raila Odinga Siasa

Imechapishwa • Imehaririwa

Raila Odinga ajiapisha kuwa rais wa Jamhuri ya watu wa Kenya

media
Kiongozi wa NASA Raila Odinga akiapa Januari 30 2018 citizentvkenya

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA Raila Odinga, amejiapisha kuwa rais wa Jamhuri ya watu wa Kenya mbele ya wafuasi wake katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi.


Odinga amechukua hatua hii licha ya onyo la serikali ya rais Uhuru Kenyatta kuwa itamfungulia mashtaka ya uhaini.

“Mimi Raila Amollo Odinga, nikiwa natambua wito, naapa kuwa rais wa Jamhuri ya watu wa Kenya,” alisema Odinga huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Kiongozi huyo aliwasili katika bustani hiyo bila ya naibu wake Kalonzo Musyoka ambaye awali aliripoti kuwa serikali ilikuwa imempokonya walinzi wake.

“Kalonzo, Mudavadi na Wetangula hawapo hapa, lakini wako pamoja nasi, mtafahamishwa ni kwanini hawakufika,” alisema Odinga

Akiwahotubia wafuasi wake, Odinga amesema wananchi wa taifa hilo wameamua kuondoa utawala wa kidikteta ulioletwa na wizi wa kura.

Aidha, amesema kuwa ametimiza ahadi aliyoitoa kwa Wakenya kuwa ataapishwa kama rais wa wananchi.