rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Tanzania Zanzibar

Imechapishwa • Imehaririwa

Tanzania yaadhimisha miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar

media
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli akisalimiana na mke wa rais wa kwanza wa Zanzibar Bi Fatuma Karume wakati wa sherehe za miaka 53 ya muungano. April 26, 2017 Ikulu/Tanzania

Nchi ya Tanzania hii leo inaadhimisha miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar, mapinduzi yaliyoshuhudia kuangushwa kwa utawala wa Sultan na familia yake January 12 mwaka 1964.


Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika huku Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ikiwa imepiga hatua katika kupambana na umasikini na kuimarisha demokrasia licha ya changamoto kadhaa za kisiasa zinazoendelea kushuhudiwa.

Wananchi wa Zanzibar wanaona siku hii inapaswa kutumiwa na Serikali kujitathmini kuangalia hatua walizopiga na changamoto ambazo zinaendelea kuikabili Zanzibar.

Zaidi ya wanamapinduzi 800 walishiriki kwenye mapinduzi hayo yaliyoifanya Zanzibar kuwa huru kutoka kwa utawala wa Kisultani.

Sherehe za leo zitajumuisha vikosi vya ulinzi na usalama nchini humo sambamba na maandamano ya wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar.

Pia kutakuepo na gwaride la vikosi vya usalama na ulinzi. Gwaride hilohilo limewaunganisha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), polisi, Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Mafunzo. Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), kikosi cha Valantia {KVZ} pamoja na kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar {KZUZ}.

Askari hao mwaka huu wamepunguza baadhi ya vitendo vinavyopamba gwaride hilo ikiwemo mwendo wa pole kwa kuzingatia kwamba tarehe 12 Januari imesimama siku tukufu ya Ijumaa ambapo waumini wa dini ya Kiislamu wamezingatiwa kupatiwa muda wa kwenda kushiriki sala ya Ijumaa.

Kilele cha sherehe za maadhimisho ya kutimia Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar kinatarajiwa kuhitimishwa Januari 12 katika Uwanja wa Aman, siku ambayo ni mapumziko ili kuwapa fursa wananchi kushiriki vyema kwenye sherehe hizo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kulihutubia Taifa Uwanjani hapo. Hotuba itakayorushwa Moja kwa moja kupitia vyombo mbali mbali vya habari nchini ikiwemo pia mitandao ya kijamii itakayowapa nafasi walimwengu Duniani kushuhudia Sherehe hizo.