Sudan Kusini: Paul Malong ni muasi wa taifa
Serikali ya Sudan Kusini imemtangaza aliyewahi kuwa mkuu majeshi Jenerali Paul Malong kama muasi wakimtuhumu kuhusika katika mashambulizi mfululizo ya juma lililopita.
Imechapishwa:
Jenerali Malong ambaye aliongoza kampeni ya rais Salva Kiir dhidi ya waasi, kwa muda mrefu alikuwa chini ya ulinzi nyumbani kwake tangu mwezi Mei baada ya rais Kiir kumfuta kazi kutokana na kujiuzulu kwa maofisa kadhaa wa jeshi wakidai kunyanyaswa na ubaguzi wa kikabila.
Hata hivyo mwezi Novemba mwaka jana rais Kiir aliruhusu jenerali Malong kutoka nyumbani kwake na kwenda kuishi uhamishoni nchini Kenya baada ya majadiliano na viongozi wa juu wa kabila la Dinka.
Msemaji wa rais Kiir, Ateny Wek Ateny anamtuhumu jenerali malong kwa kuagiza vikosi vyake kushambulia wanajeshi wa Serikali katika kile anachosema ni kutokana na ushahidi wa sauti waliounasa.
Mke wa Malong, Lucy Ayak amekashifu tangazo hili la Serikali akisema ni uongo uliotengenezwa ili kumtafutia sababu za kumshtaki mume wake.