rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

EAC Rwanda Kenya Tanzania Uganda Burundi

Imechapishwa • Imehaririwa

Wabunge wa EALA kumteua Spika mpya

media
Maafisa wa Bunge la EALA, wakiongozwa na Katibu wa Bunge hilo Kenneth Madete (Kushoto) akiwa na wageni waliomtebelea Desemba 18 2017 www.eala.org

Maslahi ya nchi ndani ya bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki EALA, yanaonekana kuzua changamoto ya kuchaguliwa wa Spika wa bunge hilo lenye makao yake mjini Arusha nchini Tanzania.


Inaaminiwa kuwa, kwa namna moja au nyingine, nchi inayotoa kiongozi huyo inanufaika kwa namna moja au nyingine, ndani ya bunge hilo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa ni rais wa Uganda Yoweri Museveni, huku nafasi ya Katibu Mkuu ikishikiliwa na Libérat Mfumukeko kutoka nchini Burundi.

Nafasi zote hizi, kiongozi husika, hukaa Ofisini mwa muda fulani na kumwachia mwingine kati ya mataifa sita ya Jumuiya hiyo, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, unasisitiza hili na kuweka wazi kuwa nyadhifa hizo zitakuwa ni za mzunguko, ili kutoa nafasi sawa kwa nchi wanachama.

Uchaguzi wa Spika, hufanywa na wabunge wa EALA na nchi inayopenda huwasilisha mgombea wake, licha ya kufahamu kuwa inaweza kukosa nafasi hiyo hasa kwa sababu nchi nyingine haijashikilia nafasi hiyo.

Hakuna shughuli zozote za bunge hilo, zinazoweza kuendelea bila kuwepo kwa Spika.

Upigaji kura ni wa siri na msimamizi wa zoezi hilo hadi kupatikana kwa Spika ni Karani wa bunge hilo.

Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kutoa Spika wa EALA kupitia, Abdulrahman Kinana, kati ya mwaka 2001-2005, baadaye Kenya ikapata nafasi hiyo kupitia Abdirahim Abdi kati ya mwaka 2007-2012.

Uganda nayo ilitoa spika Margaret Zziwa kati ya mwaka 2012-2014 huku Mganda mwingine Daniel Kidega akihudumu kati ya mwaka 2014-2017, baada ya Bi.Zziwa kuondolewa.

Mbunge wa zamani wa EALA, Peter Mathuki kutoka nchini Kenya anasema huu ni wakati wa Rwanda, ambayo haijawahi kushika wadhifa huo.

“Spika anastahili kutoka Rwanda, haiwezekani akatoka Burundi kwa sababu tayari ina Katibu Mkuu, na Tanzania tayari imewahi kutoa nafasi hiyo,” aliiambia KTN News.

Burundi, Rwanda na mwanachama mpya Sudan Kusini, tangu kuundwa kwa bunge hilo mwaka 2001, haijatoa Spika katika bunge la EALA.

Sudan Kusini ni mwanachama mpya, aliyekaribishwa mwaka 2016.

Wanaowania nafasi hiyo ni Leontine Nzeyimana, aliyekuwa Waziri wa masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Martin Ngoga kutoka Rwanda na Adam Omar Kimbisa mbunge kutoka Tanzania.

Wabunge wa Kenya na Uganda, wameafikiana kuwa watamuungana mkono mgombea kutoka Rwanda, huku Burundi na Tanzania wakionekana kuungana.

Majukumu ya bunge la EALA:-

  • Kutunga sheria zinazolenga kusaidia kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.
  • Jukumu la kwanza la bunge hilo, ni kushirikiana na mabunge ya nchi wanachama na kujadiliana kuhusu masuala ya Jumuiya.
  • Kujadili na kupitisha Bajeti ya kifedha ya Jumuiya hiyo.
  • Kuthathmini na kupitia ripoti mbalimbali za shughuli ya Jumuiya, ikiwa ni pamoja na kupitia ropoti zinazokubaliwa na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya.
  • Kutoa mapendekezo kwa namna ya kutekeleza mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.