Pata taarifa kuu
BURUNDI-SIASA-USALAMA

Rais wa Burundi azindua kampeni ya kubadilisha Katiba

Serikali ya Burundi imeanzisha kampeni tangu Jana Jumanne kuwaelezea na kuhamasisha wananchi wake kuhusu marekebisho ya katiba na kutoa maamuzi yao katika kura ya maoni.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza. REUTERS/Stringer
Matangazo ya kibiashara

Rais wa Burundi Pierre akiandamana na mkewe Denise Nkurunziza wamezindua kampeni ya kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba.

Rais Nkurunziza amesema katiba ndio inamruhusu kufanya hivyo, kwani katiba iliopo sasa haiendani na mazingira ya sasa ya nchi ya Burundi.

Wadadisi wanasema hiyo ni mbinu ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutaka kusalia madarakani, baada ya kujaribu kurekebisha mwaka 2014 kipengele cha katiba kinachomzuia kuwania muhula wa tatu bila mafanikio.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mpango huo unahusisha kuidhinishwa kwa rasimu ya katiba ambayo itamuwezesha kuwania urais kwa mihula miwili zaidi ya miaka saba kila muhula.

Kwa mujibu wa maafisa waandamizi wa chama tawala cha CNDD-FDD ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wamesema muhula wa tatu na wa mwisho kwa Nkurunziza ni huu anaohudumu hadi mwaka 2020, lakini anataka asalie madarakani hadi mwaka 2034.

Siku ya Jumanne rais Pierre Nkurunziza akiwahutubia wafuasi wake katika kijiji cha Gitega, katikati mwa Burundi, aliwaonya wale wanaopinga juhudi zake hasa wale ambao wataharisha mchakato huo kuwa watakuwa wamevuka "mstari mwekundu" na yuko tayari kukabiliana nao.

Muungano wa wanasiasa wa upinzani walio uhamishoni CNARED wamelaani maneno hayo wakisema ni kauli potovu ambazo zinalenga kuchochea machafuko nchini Burundi, huku wakisema mpango wa Nkurunziza wa kurekebisha katiba ya nchi ni kutaka asalie mamlakani. CNARED wamesem ahawatakubaliana na jambo hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.