Pata taarifa kuu
BURUNDI-SIASA

Rais wa Burundi awataka raia kuchangia fedha za uchaguzi 2020

Rais wa Burundi Piere Nkurunziza amewataka raia wa nchi hiyo kuwa tayari kuchanga fedha zitazotumiwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza RFI-Hausa by Nura
Matangazo ya kibiashara

Wito huu wa rais Nkurunziza imekuja wakati taifa hilo likiadhimisha miaka 55 ya Uhuru leo Jumamosi.

Taifa hilo la Afrika ya Kati lenye watu Milioni 11, lilipata Uhuru wake mwaka 1962 kutoka kwa wakoloni kutoka Ubelgiji.

Nkurunziza amesema wakati umefika kwa raia wa nchi hiyo kuacha kuyategemea mataifa ya Magharibi na kuamua kusimamia Uchaguzi wake mwenyewe kwa kujifadhili na fedha za ndani.

Burundi imeendelea kukabiliana na hali ngumu ya kisiasa na kiuchumi tangu mwaka 2015 baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi kutofanikiwa, baada ya Nkurunziza kuamua kuwania urais kwa muhula wa tatu kinyume na katiba ya nchi hiyo.

Maelfu ya raia wa nchi hiyo wamekimbia nchi hiyo kwa kuhofia maisha yao, wakiwemo wanaharakati, wanahabari na wanasiasa wa upinzani.

Umoja wa Mataifa hivi karibuni umesema uchunguzi wao umebaini kuwa vikosi vya usalama nchini Burundi vinaendelea kuwakamata, kuwatesa na kuwauwa raia wasiokuwa na hatia.

Hata hivyo, serikali ya Bujumbura imekuwa ikisema usalama umerejea nchini humo na kukanusha madai ya Umoja wa Mataifa na Mataifa ya Magharibi.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Michel Kafando amekuwa nchini Burundi wiki hii kuthamini hali ya kisiasa nchini humo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.