Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA waahidi mabadiliko

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, unaahidi kupambana na ufisadi, kutekeleza katiba kikamilifu, kuanzisha miradi ya kuzalisha chakula zaidi nchini humo pamoja na kuinua miundo mbinu kama barabara na reli za kisasa, iwapo mgombea wake Raila Odinga atashinda uchaguzi wa urais mwezi Agosti mwaka huu.

Vigogo wa NASA kuanzia kulia, Isaac Ruto, Kalonzo Musyoka, Raila Odinga, Musalia Mudavadi na  Moses Wetangula
Vigogo wa NASA kuanzia kulia, Isaac Ruto, Kalonzo Musyoka, Raila Odinga, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula PHOTO | JEFF ANGOTE | NATION MEDIA GROUP
Matangazo ya kibiashara

Ahadi hiyo imetolewa na Odinga, Jumanne jioni wakati akizindua Ilani ya muungano huo wa upinzani jijini Nairobi.

Waziri Mkuu huyo wa zamani pia amesema serikali yake itahakikisha kuwa fedha za umma zinatumiwa vizuri na maafisa wa serikali wanaajibika, lakini pia itakuwa ni serikali itakayosimamamia sheria.

“Tunatoa nafasi kwa Wakenya kuchagua kati ya watu waaminifu watakaotekeleza katiba yetu kikamilifu, badala ya kuendelea na wale wasiotaka mabadiliko,” Odinga aliwaambia wajumbe wa NASA.

Mbali na ahadi hiyo, NASA inaahidi kuunda nafasi za ajira kwa vijana nchini humo kwa kuanzisha kiwanda katika  Kaunti zote 47 nchini humo.

Kuhusu  Elimu, Odinga ameahidi kuwa kuanzia muhula wa tatu, wanafunzi wa Shule za Sekondari watasoma bure lakini pia watapewa mahitaji mengine muhimu kama sare na vitabu bla malipo yoyote.

Ahadi nyingine zilizotolewa na muungano wa NASA ni pamoja na kushughulikia makosa na masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu ya kihistoria, kwa kutekeleza kikamilifu ripoti ya Tume ya ukweli haki na maridhiano.

Soma pia kuhusu ahadi za chama cha Jubilee:-

Vigogo wa muungano wa upinzani nchini Kenya wakiwa katika mkutano wa kisiasa jijini Nairobi
Vigogo wa muungano wa upinzani nchini Kenya wakiwa katika mkutano wa kisiasa jijini Nairobi

Wanawake na vijana  nchini humo pia wameahidiwa kupewa nafasi kubwa katika serikali ya NASA na kutobaguliwa.

Pamoja na hilo, vita dhidi ya ukabila, ni mojawpao ya suala ambalo Odinga amesema atalishughulikia kwa kuhakikisha kuwa nafasi ya kazi zinagawanywa kwa usawa ili kuhimiza umoja wa kitaifa.

Baada ya uzinduzi wa ilani ya chama tawala Jubilee na muungano wa NASA, kampeni zinaendelea kama kawaida katika maeneo mengi ya nchi hiyo, kuelekea Uchaguzi Mkuu tarehe nane mwezi Agosti.

Dokta Brian Wanyama, mchambuzi wa siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kibabii nchini Kenya, anasema pamoja na kuzinduliwa kwa Ilani hizo, wananchi wengi huenda wasibalishe mitazamo na maamuzi  yao kwa sababu siasa za Kenya zinaegemea ukabila na ukanda.

“Itakuwa vigumu sana kwa Wakenya kubadilisha mitazamo yao kwa sababu za siasa za kikabila,” asema Wanyama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.