Pata taarifa kuu
TANZANIA-UFARANSA

AFPA: Teknolojia duni uhaba wa watu wenye ujuzi ni changamoto kwa ukuaji wa uchumi Afrika

Kukosekana kwa wafanyakazi wenye ujuzi na uhaba vifaa vya kisasa vya kufundishia kwenye vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi kunafanya nchi nyingi zinazoendelea kushindwa kuzalisha wataalamu wa kutosha watakaoajiriwa viwandani.

Meneja miradi wa ushirikiano wa kimataifa kutoka mamlaka ya mafunzo ya ufundi stadi ya nchini Ufaransa, AFPA, M-Lise Mahe akiwasilisha mada. April 5, 2017. Dar es Salaam, Tanzania
Meneja miradi wa ushirikiano wa kimataifa kutoka mamlaka ya mafunzo ya ufundi stadi ya nchini Ufaransa, AFPA, M-Lise Mahe akiwasilisha mada. April 5, 2017. Dar es Salaam, Tanzania Emmanuel Makundi/RFIKIswahili
Matangazo ya kibiashara

Haya yamesemwa wakati wa mjadala kuhusu mchango na umuhimu wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi, ambapo wataalamu wanasema vyuo hivi ni muhimu ikiwa mataifa duniani yanataka kupiga hatua zaidi na kuzalisha wataalamu wengi wataotumiwa kwenye maeneo mbalimbali yanayohitaji wataalamu.

Akiwasilisha mada kwenye mkutano wa kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania meneja mawasiliano wa mamlaka ya mafunzo na ufundi stadi VETA, Sita Peter, amesema kwa sasa taasisi yao inakabiliwa na changamoto ya vifaa vya kisasa vya kufundishia, ambapo wanalazimika kutumia gharama kubwa kununua teknolojia mpya ambayo nayo baada ya miaka mitatu au mitano inakuwa imetoka sokoni na kuingia teknolojia mpya.

Sita amesema kwa sasa wanajaribu kuwafikia watu wengi zaidi kwa kushawishi kuanzishwa kwa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi kwenye ngazi ya wilaya, ambapo ametolea mfano baadhi ya watu ambao wako mtaani na ni mafundi lakini hawakuwahi kupitia mafunzo yoyote.

“Mfano kuna watu ambao wako mtaani ni mafundi na ukiwauliza wanakwambia ni mafundi lakini hawakuwahi kupata mafunzo yoyote, kwa hiyo lengo letu sisi ni kuwaandalia hawa watu utaratibu utakaowawezesha kupata mafunzo maalumu ili kuwarasimisha na waweze kuingia kwenye mfumo wa ajira rasmi.” alisema sita.

Sita amesema VETA licha ya kuwa ina mkakati mzuri wa kutoa mafunzo kwa watu wengi zaidi ambao sasa wanahitaji mafunzo, changamoto kubwa ni uhaba wa vyuo vyenyewe na nafasi zilizopo hazitoshi kuwaingiza watu wote hawa kwa wakati mmoja.

Kwa upande wao mamlaka ya mafunzo na ufundi stadi ya nchini Ufaransa APFA, kupitia kwa meneja wake wa ushirikiano wa kimataifa, M-Lise Mahe, amesema awali walikuwa hawafahamu shughuli na mamlaka za VETA, lakini sasa anaamini baada ya kukutana na viongozi wataangalia maeneo ambayo wanaweza kushirikiana ili kufikia lengo.

Baadhi ya washiriki wa mjadala wa uwezeshaji wa sekta binafsi kupitia mafunzo ya ufundi stadi uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania. April 5, 2017.
Baadhi ya washiriki wa mjadala wa uwezeshaji wa sekta binafsi kupitia mafunzo ya ufundi stadi uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania. April 5, 2017. Emmanuel Makundi/RFIKIswahili

M-Lise amesema miongoni mwa changamoto ambazo wao kama taasisi wamezipitia na sasa nyingi ni historia, ni pamoja na pamoja na kujua mahitaji ya soko la ajira na pia kufahamu sera za uajiri na utendaji kazi wa makampuni.

Ameongeza kuwa watu wengi hasa kwenye nchi zinazoendelea wanajikuta wanaishia kufanya kazi zenye ujuzi kuliko kiwango cha mafunzo au ujuzi alionao na matokeo yake kampuni au shirika linashindwa kuwa na watendaji makini wanaofahamu vema majukumu yao.

Afpa inasema kuwa ni lazima watu waajiriwe kulingana na ujuzi walioa nao na mafunzo aliyopitia, kuliko kumfanya mtu aliyebobea kwenye masuala ya bustani, kuwa mtaalamu wa wadudu waharibifu.

“Tatizo kubwa ambao tunaliona ni kuwa baadhi ya nchi zina watu wengi ambao wako kwenye sekta rasmi na nyeti lakini hawakuwahi kupitia mafunzo yoyote ya kujengewa uwezo.” alisema M-Lise.

Amesema nchi ya Ufaransa imefanikiwa katika hili kwa sababu Serikali na sekta binafsi wanashirikiana kwa karibu sana kutengeneza mitaala ya kufundishia pamoja na kufanya tafiti za mara kwa mara kujua mahitaji ya kwenye soko na aina ya wataalamu ambao wanaweza kupelekwa.

Kwa upande wa sekta binafsi nchini Tanzania, wao wanaona kuwa bado hakuna muunganiko mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi hasa kutokana na ukweli kuwa vyuo vya mafunzo vimekuwa havizalishi vijana ambao wamekamilika na wako tayari kuingia kwenye ajira bila kuhitaji ujuzi zaidi.

Ibrahim Juma Ali ni meneja uhusiano kutoka kampuni ya Superdoll, yeye anasema vijana wengi ambao wamekuwa wakiwapokea kutoka mamlaka ya mafunzo ya ufundi stadi VETA hawana ujuzi wa kutosha kutokana na teknolojia ambazo wao wanatumia hazitumiwi na VETA kufundishia.

Juma Ali ameongeza kuwa “ni lazima VETA ibadili mtaala wake wa kufundishia na kwenda kisasa zaidi lakini kama mamlaka inapaswa kuwa na ushirikiano wa karibu na makampuni ili kuwasaidia kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wake kulingana na mahitaji ya soko na teknolojia inayotumiwa na viwanda.”

Ali anaiomba Serikali ya Tanzania badala ya kuleta wataalamu kutoka nje kuja kufanya kazi nchini, ijenge chuo cha pamoja ambacho kitakuwa na teknolojia za kisasa ili kutoa mafunzo thabiti ambayo baadae yatawasaidia kuingia kirahisi kwenye mfumo wa ajira za viwanda.

Serikali mpya ya Tanzania imeendelea kupiga kampeni na kuhamasisha kuelekea kuwa nchi ya viwanda, lakini bado changamoto kubwa ni namna ambavyo viwanda hivyo vitajengwa na tija yake lakini ni wapi pia ambako wataalamu wa hivyo viwanda vitakavyojengwa watatoka.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.