Pata taarifa kuu
KENYA

Wakenya Milioni tatu wanakabiliwa na baa la njaa

Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya linasema idadi ya wakenya wanaohitajika msaada wa chakula imeongezeka mara mbili na kufikia Milioni tatu kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Eneo lililoathiriwa na ukame Kaskazini mwa Kenya
Eneo lililoathiriwa na ukame Kaskazini mwa Kenya Yutube
Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa Shirika hilo nchini Kenya Dokta Abbas Gullet amesema idadi hiyo imeongezeka kutokana na ukame unaoendelea kushuhudiwa hasa maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Majimbo yaliyoathiriwa zaidi ni pamoja na Garissa, Isiolo, Marsabit, Kilifi, Kwale, Tana River, Lamu, Mandera, Wajir, Samburu, Turkana, West Pokot na  Baringo.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ya bara Afrika kama Ethiopia, Sudan Kusini, Somalia na Nigeria ambayo yamejipata katika janga hili ambalo linaelezwa kuwa baya zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 25.

Ukosefu wa mvua umechangia pakubwa ukosefu wa chakula kutokana na mazao kunyauka huku ukosefu wa nyasi na maji ukisababisha wafugaji kupoteza mifugo yao.

Kutokana na hali hii Shirika la msalaba mwekundu linatoa wito kwa wahisani kujitokeza kuwasaidia watu wanaoathiriwa na hali hii.

Watoto zaidi ya 300,000 wameathirika kiafya kwa ukosefu wa chakula na ikiwa hali itaendelea kuwa hivi, huenda maisha yao yatakuwa hatarini.

Mkuu wa Shirika hilo barani Afrika Fatoumata Nafo-Traore, amesema kwa sasa hakuna hata maneno yanayoweza kueleza kuhusu baa hili la njaa.

Kuna hofu kuwa ikiwa hatua ya haraka haitachukuliwa, maelfu ya watu watapoteza maisha kwa ukosefu wa chakula na maji.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.