Rais Uhuru Kenyatta kuhutubia maelfu ya wafuasi wa chama kipya cha Jubilee hii leo
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuhutubia maelfu ya wajumbe wa chama kipya cha Jubilee kilichozinduliwa rasmi hapo jana jijini Nairobi.
Imechapishwa:
Vyama zaidi ya 10 vilivyokuwa vinaunda muungano wa siasa wa Jubilee unaongoza nchini humo vilivunjwa siku ya Alhamisi na kwa mara ya kwanza wajumbe wake wamekutana jana na Naibu wa rais William Ruto.
Akiwahutubia wafuasi wa Jubilee hapo jana naibu rais William Ruto amesema kuwa tukio la kuunganisha vyama hivyo na kuwa chama kimoja inalenga kuwaleta wakenya pamoja na kuwa na chama kitakacho kuwa na ajenda ya kitaifa.
Aidha Ruto amesisitiza kuwa nia ya chama cha Jubilee ni kubadilisha siasa za chuki, utengano, ugomvi na mgawanyiko wa jamii katika nchi ya Kenya.
Chama hiki kipya cha Jubilee kinatarajiwa kutumiwa na rais Uhuru Kenyatta na naibu wake kutetea nyadhifa zao wakati wa uchaguzi Mkuu mwaka ujao.