Pata taarifa kuu
EAC

Viongozi wa EAC wakubali mapendekezo ya mratibu wa mazungumzo ya Burundi

Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameiomba Jumuiya ya kimataifa kusaidia na kufadhili mchakato wa mazungumzo ya amani kuhusu Burundi, wakati huu wakiidhinisha mapendekezo ya mratibu wa mazungumzo hayo Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto (kushoto) akiteta jambo na mwenyeji wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (Kulia) wakati walipomaliza kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, September 8, 2016
Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto (kushoto) akiteta jambo na mwenyeji wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (Kulia) wakati walipomaliza kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, September 8, 2016 Ikulu/Tanzania
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza jijini Dar es Salaam, wakati wa kuhitimisha mkutano maalumu wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais wa Tanzania na mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, John Pombe Magufuli, amesema wanaunga mkono juhudi za mratibu wa mazungumzo hayo na mpatanishi wa mgogoro wa Burundi, Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.

Rais Magufulu amesema kuwa, walipokea taarifa ya mratibu wa mazungumzo ya amani ya Burundi, Rais Mkapa, ambaye tayari ameshazikutanisha pande zinazokinzana nchini Burundi katika mazungumzo aliyoyafanya jijini Arusha na Brussels.

Mwenyekiti huyo akaongeza kuwa, baada ya kuisoma na kuisikia ripoti ya mratibu iliyokuwa na mapendekezo kadhaa kuhusu kufikia suluhu ya mzozo wa Burundi, Rais Magufuli amesema wakuu hao wa nchi kwa kauli moja wameridhia mapendekezo yake na kwamba yametoa na kuwapa picha halisi kuwa amani inakaribia kupatikana nchini humo.

Viongozi hao wameitaka Jumuiya ya Kimataifa ukiwemo umoja wa Ulaya, kusaidia kifedha mchakato wa mazungumzo hayo, ambayo wamesema bila ya uwezeshwaji wa kutosha huenda wasifikie malengo, huku wakisisitiza imani yao kwa mratibu wa mazungumzo na hatua ambazo ameshazichukua hadi sasa.

Kuhusu Sudan Kusini, wakuu hao wa nchi wameipokea rasmi kama mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika mashariki ambayo sasa itakuwa inashiriki kwenye vikao cha maamuzi ya juu ya wakuu wa nchi.

Hata hivyo viongozi hao wamesema licha ya kufurahishwa na hatua hiyo, wanaguswa na kilichotokea mwezi Julai mwaka huu, ambapo vikosi vya Serikali vilikabiliana na vile vya waasi wanaoongozwa na aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar.

Viongozi hao wametaka kukomeshwa kwa mapigano nchini humo, ambapo wamezitaka pande zinazokinzana kuweka mbele maslahi ya wananchi, na kuleta amani kwenye taifa hilo kwa ustawi wa taifa hilo changa kabisa barani Afrika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.