Pata taarifa kuu
TANZANIA

Rais Magufuli ajiandaa kukiongoza chama tawala CCM

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, anajiandaa kuchukua hatamu ya uongozi wa chama tawala nchini humo CCM, wakati wajumbe wa baraza kuu la chama watakapofanya uchaguzi mwishoni mwa juma.

Kutoka kushoto, Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete akicheka na Rais wa sasa John Pombe Magufuli
Kutoka kushoto, Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete akicheka na Rais wa sasa John Pombe Magufuli REUTERS/Emmanuel Herman
Matangazo ya kibiashara

Rais Magufuli anatarajiwa kuchukua mikoba ya kukiongoza chama hicho kutoka kwa mwenyekiti wa sasa, Jakaya Mrisho Kikwete anayemaliza muda wake.

Kabla haya ya kuelekea kwenye mkutano huu, tayari nchini Tanzania kulikuwa na mjadala kuhusu makabidhiano ya nafasi hiyo kati ya Rais Kikwete na Magufuli, ambapo kulikuwa na taarifa kuwa huenda kungefanyika mabadiliko, suala ambalo lilikanushwa na chama.

Magufuli anaenda kuchukua nafasi hiyo, wakati huu wadadisi wa masuala ya siasa wanaona kuwa, huenda kiongozi huyo akafanya mabadiliko makubwa ndani ya chama, kama ambayo yanashuhudiwa hivi sasa katika nchi.

Wataalamu wanaona kuwa huenda mrengo wa chama ukabadilika, wakati huu Magufuli, akitajwa kama mtu ambaye hakuwa na makundi ndani ya chama, na kwamba ndiye mtu pekee anayeweza kukiunganisha chama tawala ambacho kilianza kuonekana kana kwamba kuna mvutano.

Wengi wanasubiri kuona mabadiliko ambayo Rais Magufuli atayafanya pindi atakapochukua madaraka rasmi kukiongoza chama hicho.

Wakati wa kampeni, Rais Magufuli mara kadhaa alinukuliwa akiwakosoa baadhi ya wanachama na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama ambao aliwaita wasaliti, kwa kuwa walisababisha mgawanyiko kwenye chama na baadhi yao kutomuunga mkono kuhusu alichokuwa akihubiri.

Magufuli alitaka wafukuzwe ama kujiondoa wenyewe ndani ya chama, kwa watu ambao walikuwa wanaonekana kuunga mkono makundi ambayo yalitishia kukisambaratisha chama.

Siku ya Jumamosi, Julai, 23, wanachama na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi, pia watajua ni nani atakayekuwa katibu mkuu wa chama hicho kuziba nafasi ya Abdulrahman Kinana anayemaliza muda wake, au la Rais Magufuli ambakize kwenye nafasi yake.

Msemaji wa chama hicho, Chirstopher Ole Sendeka, amesema maandalizi yote kuelekea mkutano huu maalumu yamekamilika, na kwamba wajumbe wa mkutano mkuu wataanza kuwasili mjini Dodoma kuanzia wiki hii.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.