rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Kenya ICC William Ruto Fatou Bensouda

Imechapishwa • Imehaririwa

ICC kuamua kuhusu kesi ya Ruto

media
Naibu wa rais wa Kenya, William Ruto akiwa kwenye mahakama ya ICC kujibu mashtaka ya uhalifu wa kibanadamu inayomkabili Reuters

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inatazamiwa kutoa uamuzi Jumanne hii iwapo itatupilia mbali au la kesi inayomkabili Makamu wa rais wa Kenya William Ruto.


William Ruto anakabiliwa na mashtaka matatu ikiwa ni pamoja na mauaji, kuhamisha watu kwa lazima na mateso yaliyotekelezwa wakati wa vita vya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Watu wasiopungua 1,200 waliuawa wakati wa mapigano hayo.

Hata hivyo William Ruto alikana mashtaka hayo. Ruto na wanasheria wake wanataka kesi hiyo itupiliwe mbali kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Mwezi Februari Afisi ya Mwendesha mashtaka ilijaribu kutumia ushahidi wa mashahidi waliokua wamejiondoa katika kesi hiyo, lakini majaji wa Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu walitupilia mbali jambo hilo.

Waendesha mashtaka wanabaini kwamba baadhi ya mashahidi walilazimika kujiondoa katika kesi hiyo baada ya kupewa hongo na wengine kufanyiwa vitisho.

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu (ICC) Fatou Bensouda amekiri kwamba kujiondoa kwa mashahidi kumeathiri kesi dhidi ya Ruto lakini amesisitiza kwamba bado kuna ushahidi wa kutosha wa kuendelea na kesi hiyo.

Mmoja wa Wasemaji wa ICC amesema kuwa Majaji wanaweza kuondoa mashtaka yote dhidi ya Bw Ruto, wanaweza kuutaka upande wa mashtaka ubadilishe mashtaka au wanaweza kukataa tetesi za upande wa mshtakiwa na kuamua kesi iendelee.