rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Syria Marekani Uingereza Ufaransa

Imechapishwa • Imehaririwa

Trump:Tumefanikiwa katika mashambulizi yetu nchini Syria

media
Ndege ya kivita kutoka Uingereza ikishambulia Syria April 14 2018 ©REUTERS/Yiannis Kourtoglou

Rais wa Marekani Donald Trump amesifia mashambulizi ya angaa yaliyotekelezwa na wanajeshi wa nchi yake, Uingereza na Ufaransa katika maeneo yanayoaminiwa kuhifadhi silaha za kemikali nchini Syria.


Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump amesema mashambulizi hayo yalifanyika kama ilivyopangwa na lengo limetimia.

Ndege za vita za Mataifa hayo ya Magharibi yalilenga vituo viwili vya utafiti vinavyoaminiwa kuwa na silaha za kemikali, Kaskazini mwa Damascus na mjini Homs.

Urusi imelaani mashambulizi hayo na kusema yanahatarisha hali ya kibinadamu nchini Syria.

Moscow imeitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baadaye siku ya Jumamosi kujadili kilichotokea.

China nayo imelaani mashambulizi hayo na kusema pande zote zinastahili kuja katika meza ya mazungumzo na kutatua tofauti zao kwa amani.

Hata hivyo, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameunga mkono na kusifia mashambulizi hayo na kueleza kuwa yamekuja wakati mwafaka kutokana na serikali ya rais Bashar Al Assad, kuendelea kuwatesa raia wake na kuwauwa.

Wiki iliyopita, jeshi la Syria lilishtumiwa kutumia silaha za kemikali kuwashambulia raia wasiokuwa na hatia katika mji wa Douma, madai ambayo imeendelea kukanusha.