Pata taarifa kuu
KOMBE LA DUNIA BRAZIL 2014

Cameroon na Uhispania zimekuwa timu za awali kuaga michuano ya kombe la Dunia nchini Brazil

Timu ya taifa ya Cameroon wamekuwa wawakilishi wa mwanzo kabisa kutoka barani Afrika kuaga mapema zaidi fainali za kombe la dunia za mwaka huu nchini Brazil baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-0 dhidi ya timu ya taifa ya Croatia, timu ya taifa ya Uhispani ni miamba mingine toka barani Ulaya ambayo itaaga mapema michuani ya mwaka huu. 

Achille Webo (katikati) akijaribu kuwaamua wachezaji wenzake Benjamin Moukando (Kushoto) aliyekuwa akitaka kupigana na Benoît Assou-Ekotto.
Achille Webo (katikati) akijaribu kuwaamua wachezaji wenzake Benjamin Moukando (Kushoto) aliyekuwa akitaka kupigana na Benoît Assou-Ekotto. REUTERS/Murad Sezer
Matangazo ya kibiashara

Cameroon ambayo kwenye mchezo wa jana usiku ilihitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kuingia kwenye kumi na sita bora ya michuano ya mwaka huu, ilijikuta ikishindwa kufua dafu mbele ya timu ya taifa ya Croatia ambayo wachezaji wake walikuwa makini kutumia nafasi walizozipata kupachika mabao.

Marijo Mandzukic akishangilia moja ya bao aliloifungia timu yake dhidi ya Cameroon
Marijo Mandzukic akishangilia moja ya bao aliloifungia timu yake dhidi ya Cameroon REUTERS/Siphiwe Sibeko

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi, ambapo timu ya taifa ya Cameroon ilianza vema mchezo huo kwa kufanya mashambulizi ya haraka na kushtukiza kwenye lango la wapinzani wao, mashmbulizi ambayo yalionekana kana kwamba Cameroon ingeibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

Ubutu wa washambuliaji wa Cameroon walioongozwa na Vincent Aboubakar na kiungo Alender Song ambaye baadae kwenye dakika ya 40 alizwadiwa kadi nyekundu, kulitosha kuwafanya vijana hawa maarufu kama “Simba wasiofugiga” kukubali kibano cha mabao 4-0 dhidi ya Croatia ambayo safari hii tofauti na mchezo wake dhidi ya Brazil ilikuja imejipanga kwa ushindi.

Bao la kwanza la timu ya taifa ya Croatia lilipatikana katika dakika ya 11 ya mchezo likifungwa na mshambuliaji wake hatari, Ivica Olic anayekipiga na klabu ya Wolfsburg ya Ujerumani, ambapo baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Ivan Perisic hakufanya ajizi kukwamisha nyavuni mpira wa kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu ya taifa ya Cameroon ikijaribu kurejesha bao hilo bila ya mafanikio, ambapo katika dakika ya 48 ya mchezo timu ya taifa ya Croatia walifanikiwa kuandika bao la pili lililofungwa na Ivan Perisic.

Dakika ya 61 ya mchezo, Croatia wakiwa wamejipanga zaidi walifanikiwa kuandika bao la tatu kupitia kwa Mario Mandzukic anayekipiga na klabu ya Beyern Munich ya Ujerumani ambapo yeye alitumia vema mpira wa kona uliopigwa na Danijel Panjic, kabla ya dakika ya 73 ya mchezo, mshambuliaji Mario Mandzukic kuiandikia bao la ushindi timu yake.

Kwa matokeo haya sasa ni wazi wawakilishi hawa wa Afrika safari yao imetamatishwa hapo jana licha ya kusalia na mchezo mmoja kibindoni huku Croatia wenyewe wakifufua matumaini yao ya kujaribu bahati ya kuvuka kwenye hatua ya kumi na sita bora.

Kundi hili sasa linaongozwa na Brazil yenye alama 4, Mexico yenye alama 4 na Croatia ambayo baada ya ushindi wa hapo jana inajikusanyia alama 3 kwenye kundi A.

Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Uhispania, Iker Casillas akiwa hana lakufanya baada ya timu yake kufungwa
Mlinda mlango wa timu ya taifa ya Uhispania, Iker Casillas akiwa hana lakufanya baada ya timu yake kufungwa Reuters/Marcos Brindicci

Mchezo mwingine ulikuwa ni ule wa kundi B ambapo timu ya taifa ya Australia ilijitupa uwanjani kukabiliana na Uholanzi ambayo iliingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya mabingwa watetezi timu ya taifa ya Uhispania.

Kwenye mchezo huu ambao Australia itabidi wajilaumu wenyewe kwa kukosa mabao mengi ya wazi, ulikuwa ni mchezo wa kukata na shoka ambapo timu zote mbili zilionesha ufundi wa hali ya juu wa kusakata kabumbu.

Uholanzi ndio waliokuwa wa kwanza kuandika bao katika dakika ya 20 ya mchezo, bao lililofungwa na kiungo mshambuliaji Arjen Robben ambaye baada ya kupokea pasi toka kwa Daley Blind aliwazidi ujanja mabeki wa Australia na kupachika bao la kwanza.
Dakika moja baadae yaani katika dakika ya 21 ya mchezo, Australia walifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa nahodha wake mkongwe, Tim Cahill ambaye alipokea pasi kutoka kwa Ryan McGowan.

Robin Van Persie akiisawazishia timu yake ya Uholanzi bao la pili dhidi ya Australia
Robin Van Persie akiisawazishia timu yake ya Uholanzi bao la pili dhidi ya Australia REUTERS/Edgard Garrido

Katika dakika ya 54 Australia walikuja juu na kufanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Mile Jedinak ambaye alifunga bao hili kwa njia ya Penati, bao hili halikudumu sana kwani katika dakika ya 50 ya mchezo mshambuliaji hatari wa Manchester United Robin Van Persie aliisawazishia timu yake bao baada ya kutumia vema pasi aliyopewa na mchezaji Mephis Depay.

Bao la ushindi la Uholanzi lilipatikana katika dakika ya 68 ya mchezo, likifungwa na Mephis Depay ambaye akiwa nje ya eneo la hatari aliachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Australia Mat Ryan ambaye alishindwa kumudu kuudaka mpira huo.

Kwa matokeo hayo sasa Uholanzi inaongoza kundi B ikiwa na alama 6 ikifuatiwa na Chile yenye alam 6 huku Australia na Uhispania ni wazi sasa zitakuwa zimeaga rasmi michuano ya mwaka huu, na sasa zinasubiri mechi za kutamatisha ratiba ya makundi.

Leo usiku wawakilishi wengine wa Afrika timu ya taifa ya Cote d' Ivoire watatupa karata yao ya pili dhidi ya timu ya taifa ya Colombia kwenye mchezo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kwa timu zote mbili kwakuwa wote wakati wa michuano yao ya awali waliibuka na ushindi.

Mashabiki wa timu ya taifa ya Colombia
Mashabiki wa timu ya taifa ya Colombia REUTERS/John Vizcaino

Mashabiki wa soka barani Afrika wanaipa nafasi Cote d' Ivoire kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo licha ya kuwa watapata upinzani mkali toka kwa wapinzani wao timu ya taifa ya Colombia.

Mechi nyingine ni ile kati ya Uingereza na Uruguay, mechi nyingine inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka, ambapo Uingereza itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezi wao wa awali dhidi ya Italia.

Mchezo mwingine ni ule kati ya timu ya taifa ya Japan ambao watakuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Ugiriki kwenye mchezo ambao Japan itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wake wa awali dhidi ya Cote d' Ivoire.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.