rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Marekani Rwanda Linda Thomas Greenfield Joseph Nzabamwita

Imechapishwa • Imehaririwa

Jeshi la Rwanda limepuuzilia mbali vikwazo vya Kijeshi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo

media
Msemaji wa Jeshi la Rwanda Joseph Nzabamwita akizungumza na wanajeshi wa nchi hiyo

Jeshi la Rwanda limepuuzilia mbali vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo na Marekani kutokana na kuwatuhumu kuwasaidia Kundi la Waasi la M23 linalopambana na Jeshi la Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC linalotuhumiwa kuwaajiri watoto kwenye Jeshi lake.


Msemaji wa Jeshi la Rwanda Joseph Nzabamwita amesema wameshangazwa na uamuzi wa Serikali ya Marekani kuwawekea vikwazo eti kwa tuhuma za wao kuhusiska kuwafadhili Waasi wa M23 wanaosajili watoto wanaotumika kwenye Jeshi lao linaloendelea na mapigano Mashariki mwa DRC.

Marekani imeitaja Rwanda kama miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa vikiwaajiri watoto kwenye Jeshi lao kitu ambacho kimepingwa vikali na Msemaji wa Jeshi la Kigali Nzabamwita na kusema haikuwa sahihi kuwajumuisha kwenye makosa wasiyotenda.

Nzabamwita amesisitiza hiyo ni hatua ya kushangaza kwa kuwa vitendo vinavyotuhumiwa kufanywa na Rwanda hazijawahi kushuhudiwa ndani ya mipaka ya nchi hiyo kwa hiyo uamuzi huo haukuwa sahihi.

Msemaji wa Jeshi la Rwanda Nzabamwita ameweka bayana kabisa Marekani imekuwa mshirika wao mkubwa wa kijeshi kwa muda mrefu na hivyo inafahamu vilivyo ya kwamba wao wamekuwa wakipinga vikali hatua ya kuajili watoto kwenye Jeshi lao.

Jeshi la Rwanda pia limesisitiza nchi yao imekuwa mstari wa mbele kutaka amani ya kudumu irejee nchini DRC hivyo hawawezi kutoa ufadhili kwa Waasi wa M23 wanaodaiwa kufanya mkakati wa kuwaajiri watoto kwenye Jeshi lao.

Rwanda imesisitiza kuwa licha ya kuewekea vikwazo hivyo na Serikali ya Marekani lakini itaendelea kufanyakazi na taifa hilo kwa kuwa limekuwa mshirika mkubwa na wanapata msaada mkubwa wa kijeshi kutoka Serikali ya Washington.

Kauli ya Jeshi imekuja baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Anayeshughulikia Masuala ya Afrika Linda Thomas-Greenfield kutangaza vikwazo dhidi ya Rwanda baada ya kuwa na ushahidi unaodhihirisha nchi hiyo unawasaidia Waasi wa M23 wanaoajiri watoto.

Waziri Thomas-Greenfield amesema wao watasiamama kidete kutetea sheria ya kulinda watoto kuajiriwa na Jeshi ya mwaka 2008 na ndiyo maana wametaka Rwanda kuacha mara moja kuwajumuisha watoto Jeshini.

Marekani imetangaza kusitisha mafunzo yote ya kijeshi iliyokuwa inayatoa kwa Jeshi la Rwanda kipindi hiki wakiendelea na mazungumzo na Serikali ya Kigali kuhusu suala hilo la kuajiriwa kwa watoto katika Kundi la Waasi la M23.