rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Eritrea Ghana Italia Somalia

Imechapishwa • Imehaririwa

Wahamiaji Haramu kutoka Barani Afrika 94 wapoteza maisha baada ya boti yao kuzama wakielekea Nchini Italia

media
Miili ya wahamiaji haramu wapatao 94 kutoka Barani Afrika waliopoteza maisha baada ya kuzama kwa boti waliyokuwa wanasafiria

Wahamiaji haramu wapatao tisini na nne wamepoteza maisha na wengine zaidi ya mia mbili hamsini wameokolewa baada ya boti walioyokuwa wanasafiria kushika moto na kisha kuzama ikiwa njiani kuelekea katika Kisiwa cha Lampedusa kilichopo jirani na nchi ya Italia. Wahamiaji hao haramu wengi wao kutoka nchini Eritrea walikuwa wanaelekea Mataifa ya Ulaya kwa ajili ya kupata hifadhi lakini wakiwa kwenye boti yao iliyokuwa imebeba watu mia tano ilipata ajali iliyosababisha kushika moto na kuchangia kuzama kwake.


Kikosi cha Uokozi kilifika mapema na kuanza kibarua cha kuokoa manusura wa ajali hiyo ya kuzama kwa boti zoezi ambalo linatajwa kuchukua zaidi ya saa sita kabla ya kukamilika na kuwanusuru waliookoka.

Meya wa Jiji la Lampedusa Giusy Nicolini amekiri wamepokea miili ya watu tisini waliofikwa na mauti kwenye ajali hiyo ya boti iliyotokea kwenye Kisiwa jirani cha Sicilian na walipata taarifa hizo mapema asubuhi.

Taarifa zinasema boti hiyo ilikuwa imebaba wahamiaji haramu kutoka nchi za Eritrea, Somalia na Ghana wakiwa njiani kuelekea Mataifa ya Ulaya ambako walikuwa wanakwenda kusaka hifadhi.

Mamlaka za Italia zinasema licha ya kuendelea kupambana na vitendo vya wahamiaji haramu kuingia nchini humo lakini kumekuwa na changamoto nyingi zinazochangia zoezi hilo kuwa gumu kufanikiwa.

Meya Nicolini amesema wahamiaji hao walipewa taarifa za boti waliyokuwa wanasafiria kushika moto lakini wakapatwa na hamaki na hivyo wakaanza kujitosa baharini kwa lengo la kujinusuru kitu kilichochangia madhara zaidi.

Manusura wa ajali hiyo waliokolewa kisha kupewa nguo nzito kuwasitili kwa baridi lililokuwepo eneo hilo na kufyatiwa na huduma ya kwanza ili waweze kurejea kwenye hali yao ya kawaida.

Mamlaka nchini Italia zimethibitsha zitafanya mahojiano na wahamiaji hao haramu walionusurika kwenye ajali hiyo kutaka kujua walikuwa wanaelekea wapi na kina nani walikuwa wanawasaidia kuhakikisha wanafika wanakoenda.