Pata taarifa kuu
IRAN

Muda wa kupiga kura nchini Iran waongezwa

Mamilioni ya raia wa Iran wanaendelea kupiga kura  kumchagua rais mpya huku serikali ikiongeza muda wa kupiga kura kuwawezesha wananchi wengi kushiriki katika zoezi hilo la kihistoria.  

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mambo ya ndani Mostafa Moammand Najar amesema hatua ya kuongeza muda  imechukuliwa pia kwa sababu ya idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye vituo vya kupigia kura kuanzia asubuhi.

Matokeo ya awali yanatarajiwa baadaye siku ya Ijumaa au mapema siku ya Jumamosi ambapo mshindi atachukua nafasi ya rais Mahmoud Ahmadinejad anayemaliza mihula miwili baada ya kuwa mamlakani kwa kipindi cha miaka minane.

Wagombea sita wanawania kiti hicho huku watano wakielezwa kuwa wasiopenda mabadiliko isipokuwa Hassan Rowhani, ambaye amepokea uungwaji mkono katika siku za hivi karibuni kutoka kwa marais wa zamani.

Uungwaji mkono wa Rowhani, uliongezeka baada ya Mohammad Reza Aref kujiondoa baada ya kushawishiwa na waliokuwa wakati mmoja marais wa nchi hiyo Mohammad Khatami na Akbar Hashemi Rafsanjani.

Hata hivyo, Rowhani anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Saeed Jalili aliyekuwa mpatanishi wa kimataifa wa  nchi hiyo kuhusu mradi  wa Nyuklia na Meya wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf.

Kiongozi wa dini nchini humo ambaye ana mamlaka zaidi Ayatollah Khamenei anaelezwa kuwaunga mkono wagombea wengine wanaosalia na amewataka wananchi wa taifa hilo kujitokeza kwa wingi na kupiga kura.

Uchaguzi huu ni wa kwanza tangu kulipotokea kwa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2009 ambapo rais anayemaliza muda wake Ahmadinejad alituhumiwa kuiba kura.

Hakuna waangalizi wa Kimataifa walioruhusiwa kushuhudia uchaguzi huo huku vyombo vya habari vikituhumiwa kutoangazia kwa sawa kampeni za wagombea wote hao wa urais.

Mshindi anastahili kupata asilimia 50 nukta 1 ya kura zote zitakazopigwa na ikiwa hilo halitafikiwa kutakuwa na duru la pili la uchaguzi huo tarehe 21 mwezi huu.

Zaidi ya wapiga kura Milioni 50 wanashiriki katika zoezi hilo la kidemokrasia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.