rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Thailand

Imechapishwa • Imehaririwa

Afisa wa kikosi cha uokoaji afariki akijaribu kuwaokoa wavulana 12 Thailand

media
Askari wa Thailand pembezoni mwa pango ambapo wavulana 12 na kocha wao wamekwama, Julai 6, 2018. YE AUNG THU / AFP

Zoezi la kuwaokoa wavulana 12 na kocha wao waliokwama katika pango limeanza kaskazini mwa Thailand. Wavulana hao na kocha wao walikwama katika pango hilo lililofurika maji tangu siku kumi na mbili zilizopita.


Maafisa wa kikosi cha uokoaji wanajaribu kuwaokoa, lakini mmoja wao amefariki baada ya kukosa hewa akijaribu kuingia katika pango hilo. Hali ambayo imezua wasiwasi ya kuwaokoa haraka watoto hao. Maafisa wa uokoaji wanajaribu kuondoa maji katika pango hilo kabla mvua hazijaanza tena kunyesha.

Afisa huyo aliyefariki ni mmoja wa askari wa zamani wa kikosi cha jeshi la wanamaji, ambaye alifariki kwa kukosa hewa baada ya kupiga mbizi kwa muda wa saa kumi na mbili usiku wa kuamkia Ijumaa hii, Julai 6 wakati alikua akishiriki katika operesheni ya kujaribu kuwaokoa wavulana hao 12 na kocha wao ambao bado wamekwama katika pango ikiwa leo imeingia siku ya kumi na tatu.

Mfalme wa Thailand ametangaza kwamba atashiriki mazishi ya afisa huyo. Tukio hilo limezua wasiwasi kwa viongozi wa Thailand ambao walikua na imani kwamba zoezi hilo lingefanyika haraka na kuweza kuwaokoa wavulana hao na kukocha wao.

"Tumeanza kuweka mitungi ya oksijeni katika pango," amesema Direk Taptim, mmoja wa maafisa wa uokoaji. Na maji yameanza kupungua baada ya kuyaondoa kwa kutumia chombo maalumu, ameongeza Bw Derik.