rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Korea Kaskazini Marekani Donald Trump Kim Jong Un

Imechapishwa • Imehaririwa

Vita ya Korea: mabaki ya askari 200 wa Marekani yakabidhiwa

media
Trump alisema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa Korea Kaskazini imekubali kukabidhi mabaki ya askari wa Marekani. REUTERS

Korea ya Kaskazini imekabidhi Marekani mabaki ya askari wake 200 waliotoweka wakati wa Vita ya Korea, Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza, taarifa ambayo haijathibitishwa na jeshi la Marekani.


"Tumepokea mashujaa wetu wote waliofariki, mabaki yamerejeshwa nyumbani leo, tayari miili ya askari 200 imerejeshwa nyumbani," amesema rais wa Marekani kwa wafuasi wake wakati wa mkutano wa hadhara katika mji wa Duluth, Minnesota Jumatano wiki hii.

Maafisa wa Marekani walisema siku ya Jumanne kuwa Korea Kaskazini itakabidhi katika siku zijazo "idadi kubwa" ya miili ya askari wa nchi hiyo kwa uangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Korea Kusini na kisha miili hiyo itasafirishwa katika kambi ya kijeshi ya Hickam, katika jimbo la Hawaii.

Baada ya mkutano wa kihistoria wa Juni 12 na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, Donald Trump alisema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa Korea Kaskazini imekubali kukabidhi mabaki ya askari wa Marekani.

Takribani askari wa Marekani 7, 700 walitoweka tangu Vita ya Korea (1950-1953), kulingana na takwimu zilizotolewa na Marekani. Maofisa wa Korea Kaskazini walisema siku za nyuma kuwa wanahifadhi mabaki ya askari 200 wa Marekani, kwa mujibu wa Pentagon.

Zaidi ya askari 36,500 Marekani waliuawa katika vita.

Mabaki ya askari wa Marekani yalikabidhiwa mara ya mwisho mwaka 2007, wakati wa ziara ya gavana wa New Mexico wakati huo, Bill Richardson, mjini Pyongyang.