rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Brazili Majanga ya Asili Jair Bolsonaro

Imechapishwa • Imehaririwa

Amazon: Baada ya shinikizo la kimataifa, Brazili yatuma jeshi kukabiliana na moto

media
Mwanaharakati akibebelea bango lililoandikwa: "Kila kinachotokea duniani, kitatokea kwa watoto wa dunia", kwenye pwani ya Ipanema, Rio, Agosti 25. MAURO PIMENTEL / AFP

Kufuatia shinikizo la kimataifa, Brazili imetuma jeshi lake kukabiliana na moto, ambao umeendelea kushika kasi na kuathiri maeneo kadhaa ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa nchini Brazili, uamuzi huo umechukuliwa kwa dharura.


Maandamano yalifanyika katika miji kadhaa ya Brazil kwa minajili ya kuimarisha ulinzi katika msitu wa Amazon na dhidi ya Rais Jair Bolsonaro ambaye alikuwa hajachukuwa hatua zozote kwa kukabiliana na moto huo. Lakini mabishano ya kidiplomasia kati ya Ufaransa na Brazil yanazidi kuongezeka. Ubalozi wa Ufaransa mjini Brasilia hata hivyo umelengwa.

Maandamano kwa niaba ya msitu wa Amazon yamekusanya maelfu ya watu katika miji kadhaa mikubwa ya nchi hiyo kama Rio, kwa uungwaji mkono wa viongozi kadhaa, wasanii na wanasiasa wa mrengo wa kushoto. Maandamano ya kukemea kushindwa kwa rais Jair Bolsonaro kukabiliana na moto huo.

Hivi karibuni Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema kuwa idadi ya maafa ya moto katika msitu wa Amazon ni janga la kimataifa ambalo linapaswa kujadiliwa katika mkutano wa nchi zenye nguvu kiuchumi maarufu kama G7.

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro alijibu maneno hayo ya Macron akidai kuwa anatumia janga hilo kisiasa.

Ameongeza kuwa kujadili janga la moto katika mkutano wa G7 na Brazil haipo ni kama kuleta ukoloni.

Amazon ni Msitu mkubwa zaidi Duniani, ambao unasaidia kupunguza kasi ya ongezeko la joto.

Takribani asilimia 20 ya hewa safi duniani kote huzalishwa kutoka kwenye msitu huo.

Makundi ya wana mazingira wameitisha maandamano katika miji mbalimbali nchini Brazil siku ya ijumaa kutaka hatua zichukuliwe kuzuia moto huo.

Msitu wa Amazon ni msitu mkubwa uliopo katika bonde la tropiki la Mto Amazon.

Una eneo la takribani kilomita za mraba milioni saba, ambazo kati yake tano na nusu zimefunikwa na msitu wa mvua.

Msitu huo unajumuisha mataifa tisa: uko ndani ya Brazil kwa asilimia 60, ikifuatiwa na Peru asilimia 13, na Colombia asilimia 10, halafu Venezuela, Ecuador, Bolivia, Guyana, Suriname na Guyana ya Kifaransa kwa kiasi kidogo.