Korea Kaskazini yataka mazungumzo na Marekani kuendelea
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, anataka mkutano wake na rais wa Marekani Donald Trump kuendelea mwezi ujao nchini Singapore kama ilivyopangwa.
Imechapishwa:
Kim Jong Un, amekutana na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in, ambaye amesema uongozi wa Korea Kaskazini bado una nia ya kutokuwa na maeneo ya kutengeza silaha za nyuklia.
Kauli hii ya kiongozi huyo wa Kaskazini, imekuja wakati huu rais Trump akisema bado wanaendelea kuzungumza na maafisa wa Pyongyang na huenda mazungumzo hayo yakaendelea kama ilivyopagwa.
Wiki hii, rais Trump alijiondoa kwenye mazungumzo hayo, baada ya kusema kuwa, matamshi yenye ukali na yaliyoonekana kuwa ya chuki, kutoka Korea Kaskazini yasingemwezesha kuja katika meza ya mazungumzo.
Hata hivyo, matamshi ya rais Trump siku ya Jumamosi kwamba mambo yanakwenda vizuri, huenda viongozi hao wakakutana tarehe 12 mwezi Juni kama ambavyo ilikuwa imepangwa.
Korea Kaskazini pamona na kutaka mkutano huo, imeonekana kutokubaliana na msimamo wa Marekani kuwa iachane kabisa na mradi wake wa nyuklia, suala ambalo linaendelea kuwa tata.