rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Donald Trump Marekani Urusi Uchaguzi Marekani 2016

Imechapishwa • Imehaririwa

Trump akanusha taarifa za kutaka kumfuta kazi Mueller

media
Donald Trump rais wa Marekani REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa kuwa anapanga kumfuta kazi mkuu wa jopo maalimu la uchunguzi Robert Mueller ambaye anachunguza uwezekano kuwa Urusi iliingilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2016.


Kumeripotiwa kuibuka mvutano na sintofahamu kubwa kati ya ikulu ya rais Trump pamoja na kamati ya uchunguzi inayoongozwa na Mueller.

Siku ya Jumamosi mmoja wa mawakili wa rais Trump alinukuliwa akidai kuwa timu ya Mueller ilichukua maelfu ya barua pepe kinyume cha sheria.

Alipoulizwa kuhusu mtafaruku wa kisheria uliojitokeza kati ya ofisi yake na timu ya Mueller, rais Trump alijibu kwa kudai kuwa hali sio shwari na timu yake imekasirishwa na namna Mueller amekuwa akipata baadhi ya taarifa.

Rais Trump amesema "sidhani kama kuna kitu wanacho, kwasababu navyoongea hapa hakukuwa na kuingiliwa kwa uchaguzi wetu".

Utawala wa rais Trump hata hivyo umekanusha madai kuwa umekuwa ukifanya kazi kwa karibu na nchi ya Urusi kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2016 ambao ulishuhudia rais Trump akimbwaga mgombea wa Democrat Hillary Clinton.

Wabunge kadhaa wa Democrat tayari wameeleza kuguswa na matamshi ya Trump ambapo juma lililopita mjumbe wa kamati ya sheria kutoka chama cha Democrat Adam Schiff amesema wabunge wa Republican wamepanga kuzima uchunguzi huu.

Wafanyakazi kadhaa wa timu ya kampeni ya Trump wanakabiliwa na kesi mahakamani wakiwa katika sehemu ya uchunguzi unaoendelea kufanywa na Mueller.