Pata taarifa kuu
DRC-TSHISEKEDI-MAWAZIRI-SIASA

Rais wa DRC Felix Tshisekedi atishia kuwafuta kazi Mawaziri

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Félix Tshisekedi ametishia kuwafuta kazi Mawaziri wake na hata kulivunja bunge, iwapo washirika wake wa kisiasa ambao wanaegemea katika mrengo wa rais wa zamani Joseph Kabila, wataendelea kumdharau.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi Sumy Sadurni / AFP
Matangazo ya kibiashara

Tshisekedi amesema kuna baadhi ya Mawaziri ambao wamekuwa wakimwambia kuwa, wanapata shinikizo, na kusisitiza kuwa, hana nia ya kulivunja bunge lakini, iwapo mzozo utazuka, atalazimika kufanya hivyo.

“Ninayoyasema ndio ambayo yatafanyika, na ambayo nimedhamiria kufanya ndio yatakayotekelezwa, sababu raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamenipa jukumu la kuwaongoza na bila shaka wataniuliza nini nimewafanyia kwa muda wa miaka mitano, ” alisema.

“Wamenipa taabu sana wanasubiri nishindwe kutimiza kazi yangu, wananisukuma kufanya mambo ambayo sijapanga kufanya, kama ni kuvunja bunge naweza kulivunja, na kama itabidi nifikie hatua hiyo sitachelewa kufanya hivyo,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Tshisekedi ametupilia mbali madai ya kuwepo mpango wa kuigawa nchi hiyo, akisema mazungumzo hayo hayana msingi na ni mbinu za kutaka kuchelewesha ajenda ya maendeleo kwa taifa hilo.

Aidha, amesema anashangazwa na namna ambavyo baadhi ya watu wanataka kulikuza suala la kuigawa vipande nchi hiyo, kiongozi huyo akisisitiza kuwa hakuna atakayejaribu kufanya hivyo.

Matamshi yake yamekuja baada ya majuma kadhaa yaliyopita baadhi ya wanasiasa kuzituhumu nchi za ukanda na baadhi ya wanasiasa wa DRC kutaka kuligawa vipande eneo la mashariki mwa DRC.

Rais Tshisekedi ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, aliingia katika maelewano na chama cha zamani wa rais Kabila cha PPRD, kushirikiana naye katika serikali yake, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2018.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.