Ugiriki yataka kusaidia kuokoa mchakato wa amani Libya
Ugiriki inasema inataka pia kuhusishwa katika mzozo wa Libya, wakati huu Uturuki ikionekana kuchukua usukani wa kulisaidia taifa hilo la Afrika Kaskazini kuwa salama.
Imechapishwa:
Kauli ya Ugiriki, imetolewa na serikali ya nchi hiyo ambayo inasema iwapo haitahusika, huenda eneo la Meditterian likaathirika na mzozo huo. Kwa upande mwengine Uturuki inasema inataka kutuma jeshi lake kuisaidia serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa, dhidi ya makundi ya wapinzani.
Hayo yanajiri wakati serikali ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imekanusha kuwa inasaidiwa na kikosi cha waasi wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki ametahadharisha kwamba mgogoro wa nchini Libya unaweza kutumbukia katika vurumai na kwamba nchi hiyo inaweza kugeuka Syria nyingine. Waziri huyo Mevlut Cavusoglu amesema hayo wakati akifanya juhudi kwa lengo la kupitisha sheria ya kuiwezesha Uturuki kupeleka majeshi nchini Libya.
Waziri Cavusoglu amesema ikiwa Libya itageuka kuwa Syria nyingine na nchi zote za kanda zitaathirika
Serikali ya Libya inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa imekuwa inakabiliana na majeshi ya jenerali muasi Khalifa Haftar yanayoungwa mkono na Urusi, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Jordan.
Majeshi ya Jenerali muasi Haftar mpaka sasa bado hayajaweza kuingia mjini Tripoli lakini taarifa zinasema vikosi vyake vimepata mafanikio ya kiasi fulani kusinimwa mji huo kutokana na msaada wa wapiganaji kutoka Urusi na Sudan.