Uganda na DRC zakubaliana kushiriki katika masuala ya usalama na biashara
Mataifa jirani ya Uganda na DRC yamekubaliana kushirikiana katika mikataba kadhaa ya maendeleo na usalama.
Imechapishwa:
Umekuwa ni mkutano wa kwanza wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili, na kuhudhuria rais Felix Tshisekedi akiambatana na ujumbe wa watu 117 wakiwemo Mawaziri.
Miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa katika mkutano huo ni kwa Kampala na Kinshasa kushirikiana katika masuala ya miundo mbinu, biashara na uwezekaji pamoja na ulinzi na usalama.
Katika mkutano huo, rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema, anaunga mkono ombi la DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuungana na mataifa mengine kama Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.
Uhusiano wa Uganda na DRC katika miaka iliyopita, ulionekana kuwa mbaya lakini tangu kuingia madarakani kwa rais Tshisekedi mwezi Januari, mambo yameanza kubadilika huku nchi hizo mbili zikiahidi kushirikiana zaidi.
Baada ya ziara yake nchini Uganda, rais Tshisekedi anakwenda jijini Paris kukutana na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.