ECOWAS: Hatua ya José Mario Vaz ya kuvunja serikali ni kinyume na sheria
Taarifa ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, iliyotolewa Jumanne wiki hii inabaini kwamba serikali iliyovunjwa Jumatatu na Rais José Mario Vaz ni matokeo ya uamuzi wa mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo uliyofanyika Juni 29, 2019.
Imechapishwa:
Mkutano huo, ECOWAS inasema, ulibaini kwamba muhula wa José Mario Vaz ulimalizika mwishoni mwa Juni, na hiyo inaweza kusababisha kukosekana kwa serikali halali na hivyo kusababisha mkwamo katika shughuli za serikali.
Wakati huo huo ECOWAS inaona kwamba hatua ya Rais José Mario Vaz ya kuvunja serikali ni kinyume cha sheria wakati hana mamlaka yoyote ya kuchukuwa hatua yoyote ile.
ECOWAS katika taarifa yake inasema inauunga mkono timu ya waziri mkuu aliyefukuzwa kazi Aristide Gomez na inamtaka waziri huyo mkuu kuendelea na maandalizi ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Novemba 24.
ECOWAS imebaini kwamba ikiwa zimesalia wiki tatu kabla ya uchaguzi, hakuna sababu ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi, hali ambayo inaweza kusababisha nchi inatumbukia katika machafuko zaidi.
"Mtu yeyote ambaye kwa njia yoyote atahatarisha mchakato wa uchaguzi, atakabiliwa na vikwazo," ECOWAS imeonya.