rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Afrika Kusini Nigeria Julius Malema

Imechapishwa • Imehaririwa

Mvutano kati ya Afrika Kusini na Nigeria: Sekta ya uchumi yaangiliwa na wasiwasi

media
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa katika mkutano wa kiuchumi wa dunia Septemba 5, 2019, Cape Town. REUTERS/Sumaya Hisham

Nigeria imeahidi kushirikiana na Pretoria kujaribu kumaliza ghasia zinazochochewa na chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini. Mvutano kati ya nchi hizi mbili unatokea wakati Nigeria na Afrika Kusini zina uhusiano mzuri kiuchumi.


Mvutano uliibuka katika siku za hivi karibuni kati ya nchi hizi mbili zenye uchumi mkubwa barani Afrika. Baada ya ghasia za chuki dhidi ya wageni kushuhudiwa katika miji kadhaa ya Afrika Kusini, baadhi ya raia wa Nigeria walishambulia makampuni na majengo ya serikali ya Afrika Kusini nchini Nigeria, hadi mashirika kadhaa kama vile kampuni ya simu ya MTN kuamua kufunga milango kwa kuhofia kuporwa, wakati ghasia zilizuka mapema wiki hii mbele ya maduka kadhaa ya kampuni ya Shoprite kutoka Afrika Kusini nchini Nigeria.

Wakati huo huo Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kufunga kwa muda ubalozi wake jijini Abuja na Lagos nchini Nigeria, kufuatia visa vya ulipizaji kisasi kwa makampuni yake nchini humo.

Siku ya Jumatano kulikuwa na maandamano jijini Abuja, kulaani kile walichokiita ndugu zao kuuawa nchini Afrika Kusini na hadi sasa watu saba wameuawa.

Baadhi ya mitambo ya kampuni ya mawasiliano ya MTN ziliteketezwa moto huku maduka ya jumla ya Shoprite yakivamiwa na waandamanaji waliokuwa na hasira nchini Nigeria.

Julius Malema, kiongozi wa chama cha upinzani cha EFF amewalaumu Wazungu kwa ghasia zinazotokea.

Kuanzia Jumapili iliyopita, maduka ya raia wa Nigeria na wageni yameendelea kuvamiwa na bidhaa kuporwa jijini Johannesburg.