Pata taarifa kuu
SUDAN

Sudan: Waandamanaji na wanajeshi wakubaliana kuanza tena mazungumzo

Viongozi wa waandamanaji wamekubali kusitisha mgomo wao wa nchi nzima waliouanzisha juma hili baada ya vyombo vya usalama kuwaondoa kwa nguvu waandamanaji kuzingira makao makuu ya jeshi ambapo watu kadhaa walipoteza maisha.

Wanajeshi wa kikosi maalumu cha kukabiliana na wahalifu wakipiga doria kwenye mitaa ya Khartoum. Juni 10, 2019
Wanajeshi wa kikosi maalumu cha kukabiliana na wahalifu wakipiga doria kwenye mitaa ya Khartoum. Juni 10, 2019 (AFP)
Matangazo ya kibiashara

Mbali na kutangaza kusitisha mgomo wa kuisusia Serikali, viongozi hao pia wamekubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo na viongozi wa baraza la kijeshi na hii ni kwa mujibu wa wapatanishi kutoka Serikali ya Ethiopia.

Makubaliano haya ambayo hata hivyo uongozi wa kijeshi haujathibitisha, yamekua wakati huu mwanadiplomasia wa Serikali ya Marekani akianza ziara nchini humo kujaribu kuwashawishi wanajeshi kuacha kutumia nguvu kukabiliana na waandamanaji.

Nchi ya Sudan imekuwa chini ya uongozi wa kijeshi tangu kuondolewa madarakani kwa Omar al-Bashir, April 11 mwaka huu baada ya miezi kadhaa ya maandamani dhidi ya kumalizika kwa utawala wake wa miongo mitatu.

Baada ya Bashir kuondolewa madarakani waandamanaji walipiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum kwa majuma kadhaa wakishinikiza kuwekwa kwa utawala wa kiraia, kabla ya wanajeshi wa kikosi maalumu kuwasambaratisha Juni 3 ambapo watu zaidi ya 100 wameuawa.

Jumapili ya wiki iliyopita viongozi wa waandamanaji walitangaza kuanza kwa mgomo wa nchi nzima wa kutotii Serikali wakitaka kwanza kuwajibishwa kwa wanajeshi waliohusika na mauaji ya raia ndip wafikirie kuendelea na mazungumzo.

Waandamanaji juma hili wameongeza shinikizo zaidi kwa viongozi wa kijeshi kuwaachia viongozi wao ambao walikamatwa mwishoni mwa juma na wale waliokamatwa wakati wa maandamano.

Mjumbe wa Serikali ya Ethiopia inayosimamia mpango wa kutafuta suluhu ya kisiasa nchini humo, amesema kumefikiwa makubaliano kati ya viongozi wa kijeshi na waandamanaji ambapo sasa watarejea kwenye meza ya mazungumzo.

Hatua hii imekuja baada ya ziara iliyofanywa mwishoni mwa juma na waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ambaye alikutana na viongozi wa pande zote mbili.

Viongozi wa waandamanaji sasa wanataka mbali na kufanyika kwa mazungumzo mapya, jeshi liwaachie wafungwa wote wa kisiasa wanaoshikiliwa.

Katika hatua nyingine baraza la usalama la umoja wa Mataifa katika kikao chao cha Jumanne ya wiki hii, limekashifu vikali jeshi la Sudan kwa kutumia njia zisizo za kawaida kukabiliana na waandamanaji kwenye miji mbalimbali nchini humo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.