Pata taarifa kuu
BOTSWANA

Mahakama ya Botswana yabatilisha sheria inayokataza mapenzi ya jinsia moja

Nchi ya Botswana imekuwa ni taifa jingine la Afrika ambalo limeruhusu mapenzi ya jinsia moja baada ya mahakama kuu kutupilia mbali kipengele cha katiba ambacho kilikuwa kinakataza na kuadhibu hadi kifungo cha miaka 7 jela kwa watu watakaojihusisha na ushoga.

Mtu akipita katika eneo lenye rangi zinazotumiwa na watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja "ushoga".
Mtu akipita katika eneo lenye rangi zinazotumiwa na watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja "ushoga". GEORGES GOBET / AFP
Matangazo ya kibiashara

Punde baada ya uamuzi huo wa mahakama, wanaharakati wanaotetea mapenzi ya jinsia moja walisikika wakishangilia ndani ya ukumbi wa mahakama baada ya majaji wote waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo kuridhia pasi na shaka kuondolewa kwa kipengele hicho cha sheria.

Uamuzi wa mahakama ya Botswana umekuja wakati huu karibu nusu ya mataifa yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara yanasheria kali zinazokataza mapenzi ya jinsia moja.

Mapema mwaka huu nchi ya Angola na yenyewe iliruhusu mapenzi ya jinsia moja ikifuta sheria ya awali iliyokuwa ikilitaja kuwa kosa la jinai kwa mtu au watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja maarufu kama Ushoga.

Waliowasilisha kesi mahakamani walidai kuwa sheria zilizokuwepo zilitungwa wakati wa ukoloni na kwamba watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wamekuwa wakitengwa na wakati mwingine maisha yao kuwa hatarini.

Shirika lisilo la kiserikali nchini Botswana la LEGABIBO ambalo lilishiriki katika kuwasilisha pingamizi mahakamani kupinga sheria zilizopo, limesema sheria za awali ni wazi zilikuwa zinakiuka haki za binadamu.

Hata hivyo licha ya uamuzi huu wa Botswana uliopokelewa kwa shangwe, wanaharakati wengi bado wamechukizwa na uamuzi wa mahakama kuu ya Kenya ambayo ilisisitiza kuwa mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria.

Mahakama ya Botswana kwenye uamuzi wake imesema, kuwaadhibu watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja kwa sababu tu ndivyo walivyo ni kutowatendea haki na kutowaheshimu na kwamba sheria haipaswi kuingilia masuala ambayo ni ya watu binafsi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.