rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Algeria Abdelaziz Bouteflika Siasa

Imechapishwa • Imehaririwa

Rais wa mpito nchini Algeria aitisha mazungumzo ya kitaifa

media
Rais wa mpito nchini Algeria Abdelkader Bensalah Télévision nationale algérienne/AFP

Rais wa mpito nchini Algeria, Abdelkader Bensalah ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa nchini humo, baada ya kuonekana wazi kuwa itakuwa vigumu sana kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa tarehe 4 mwezi Julai.


Bensalah amewataka wanasiasa wote na mashirika ya kiraia, kuja pamoja ili kuwa na sauti moja na kupanga tarehe mpya ya Uchaguzi Mkuu.

Algeria iliingia katika mzozo wa kisiasa baada ya kushinikizwa kujiuzulu kwa rais wa zamani Abdelaziz Bouteflika na waandamanaji kumkata rais wa mpito.

Tangu kuondolewa madarakani kwa rais Bouterflika, nchi hiyo imeendelea kushuhudia maandamano mfululizo, wananchi wakitaka kujiuzulu kwa viongozi waliohudumu chini ya utawala wake.

Tarehe 22 mwezi Februari, maelfu ya watu walianza kuandamana jijini Algiers na miji mingine kupinga hatua ya Bouteflika kutangaza kuwania tena urais kwa muhula wa tano baada ya kuongoza nchi hiyo kwa miaka 20.

Bouteflika mwenye umri wa miaka 82, aliyekuwa anasumbuliwa na kiharusi tangu mwaka 2013 alikuwa hajawahi kuonekana hadharani kwa kipindi kirefu.

Siku moja baada ya kurejea nyumbani akitokea Uswisi alikokuwa ameenda kupata matibabu, Bouteflika tarehe 11 mwezi Machi alitangaza kutowania tena urais.

Baada ya shinikizo za wananchi na baadaye jeshi kuingilia kati, tarehe 2 mwezi Aprili, Bouteflika alitangaza kujiuzulu kama rais wa nchi hiyo, hatua ambayo iliwafurahisha raia wa taifa hilo la Afrika Kaskazini.