Pata taarifa kuu
SUDAN-MAUAJI-SIASA-WAANDAMANAJI-AU

Umoja wa Afrika waifungia Sudan, walitaka jeshi kukabidhi madaraka kwa raia

Umoja wa Afrika umeifungia Sudan kuwa mwanachama wa umoja huo, na kulitaka uongozi wa kijeshi kukabidhi madaraka kwa raia, baada ya maafisa wa usalama kuwauwa raia 100 wiki hii.

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat African Union on Twitter
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imechukuliwa baada ya kikao cha Baraza la amani na usalama cha Umoja huo, tangazo ambalo limetangazwa kupitia ukurasa wake wa Twitter na hii inamaanisha kuwa Sudan sio mwanachama wa Umoja huo.

Baraza hilo linasema njia pekee ya kuirejesha Sudan kuwa mwanachama wa umoja huo wenye nchi 55, ni kuwa na serikali ya kiraia.

Umoja wa Afrika sasa unataka jeshi kuhakikisha kuwa inakabidhi madaraka kwa amani, haraka iwezekanavyo.

Hali ilivyo jijini Khartoum Juni 04 2019
Hali ilivyo jijini Khartoum Juni 04 2019 REUTERS/Stringer

Wakati hayo yakijiri, Wizara ya afya nchini Sudan inasema watu walipoteza maisha kutokana na makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama wiki hii jijini Khartoum, hawazidi 46.

Naibu Waziri wa afya Suleiman Abdul Jabbar, amekanusha ripoti ambazo zimekuwa zikitolewa na Madaktari na wanaharakati kuwa, watu waliopoteza maisha ni zaidi ya 100.

Pamoja na hayo, viongozi wa waandamanaji nchini Sudan wamekataa wito wa mazungumzo uliotolewa na watawala wa kijeshi, wakitaka haki ipatikane dhidi ya wanajeshi waliohusika na mauaji ya raia.

Wito wa jeshi unakuja ikiwa siku nne zimepita tangu litangaze kusitisha mazungumzo na waandamanaji pamoja na kufuta makubaliano yote yaliyokuwa yamefikiwa katika mazungumzo ya awali.

Hali ya machafuko jijini Khartoum nchini Sudan
Hali ya machafuko jijini Khartoum nchini Sudan ASHRAF SHAZLY / AFP

Jumatatu ya wiki hii, vyombo vya usalama nchini humo vilitumia nguvu kubwa kuwaondoa maelfu ya raia waliokuwa wamepiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi, ambapo watu zaidi ya 100 wameuawa na wengine mamia kujeruhiwa.

Wapiganaji wa waasi kutoka kundi la Janjaweed wanatuhumiwa kuhusika katika utekelezaji wa vitendo vya unyanyasaji wa raia ikiwemo kuwatesa, kuwaua na kuwabaka wanawake kadhaa.

Msemaji wa Baraza la wasomi ambalo linaongoza maandamano hayo, Amjad Farid amesema wananchi hawako tayari kwa mazungumzo na wanajeshi kwa kile alichosema hawaamini huku akitaka kwanza waliohusika na mauaji pamoja na unyanyasaji wa raia wakamatwe.

Kiongozi wa kijeshi nchini Sudan Abdel Fattah al-Burhan Abdulrahman
Kiongozi wa kijeshi nchini Sudan Abdel Fattah al-Burhan Abdulrahman AFP

Hali hiyo imeendelea kusababisha kutanda kwa hali ya wasiwasi nchini humo, wakati huu jeshi likiwa limetangaza kuwa Uchaguzi nchini humo utafanyika baada ya miezi tisa, lakini waandamanaji wamekataa hilo.

Mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yamelaani hatua ya uongozi wa kijeshi kuamua kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.