Pata taarifa kuu
CAR-ICC

Mbunge na kiongozi wa waasi Jamhuri ya Afrika ya Kati afikiswaha ICC

Kiongozi wa zamani wa waasi aliyefahamika kama “Kanali Rambo” nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, amewasili hapo jana katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC iliyoko The Hague nchini Uholanzi, ambako anashtakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita na dhulma dhidi ya binadamu.

Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC.
Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC. ICC-CPI
Matangazo ya kibiashara

Alfred Yekatom ambaye kwa sasa ni mbunge, amekuwa mtuhumiwa wa kwanza wa aina yake kusafirishwa kwenda katika mahakama ya ICC.

Msemaji wa mahakama ya ICC, Fadi El Abdallah amethibitisha kupokelewa kwa mtuhumiwa huyo na kuongeza kuwa tayari anazuiliwa kwenye jela maalumu ya mahakama hiyo.

Rambo alikuwa amelengwa na vikwazo kutoka nchi ya Marekani mwaka 2015 kwa tuhuma za kuwashambulia waislamu, kusababisha vifo vya raia na kutumia watoto kama wanajeshi.

Baada ya kuchaguliwa kuingia bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2016, Yekatom mwenye umri wa miaka 43, alikamatwa mwezi October mwaka huu baada ya kufyatua risasi ndani ya bunge wakati spika mpya alipokuwa akiapishwa.

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda amekaribisha kusafirishwa kwa mtuhumiwa huyo ambapo amesema hatua hii itatoa haki kwa raia wa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamepokea kwa mtazamo chanya kusafirishwa kwa Yekatom kwenye mahakama ya ICC, mashirika haya yakisema hatua hii inatuma ujumbe kwa viongozi wengine wa makundi ya waasi.

Mahakama ya ICC inasema kuwa Yekatom atashtakiwa kwa tuhuma za makosa ya uhalifu wa kivita na dhulma dhidi ya binadamu aliyoyatekeleza wakati akiwa kiongozi wa kundi la waasi wa Anti-Balaka.

Mahakama hiyo ilianzisha uchunguzi wake mwezi September mwaka 2014 dhidi ya uhalifu uliotekelezwa tangu nchi hiyo ishuhudie machafuko kuanzia mwaka 2012.

Majaji watatu wa mahakama hiyo walitoa waranti ya kukamatwa kwa Yekatom, Jumapili ya wiki iliyopita.

“Mahakama imejiridhisha kuwa ushahidi wa awali uliowekwa mezani unathibitisha pasipo na shaka kuwa Yekatom anawajibika kutokana na makosa aliyoyatekeleza.” walisema majaji wa mahakama hiyo wakati wakitoa waranti ya kukamatwa kwake.

Miongoni mwa makosa yanayomkabili ni pamoja na mauaji, mateso, na kutumia watoto walio na umri wa chini ya miaka 15 kwenye jeshi lake la anti-balaka kati ya Desemba 5 2013 na August 2014.

Wakati nchi hiyo ikiendelea kushuhudiwa machafuko siku ya Ijumaa mwanajeshi mmoja wa kulinda amani kutoka Tanzania aliuawa katika shambulio lililotekelezwa na waasi kulenga kambi ya umoja wa Mataifa kwenye kambi ya Ghambia.

Mwishoni mwa juma umoja wa Mataifa umesema watu 37 waliuawa katika vurugu za juma lililopita akiwemo mchungaji aliyepatikana amezikwa, baada ya kundi jipya la waasi linalofahamika kam Sirri kutekeleza mashambulizi mfululizo.

Vurugu hizi zlianza siku ya Alhamisi baada ya waumini wa Kikristo kumuu muumini wa Kiislamu tukio ambalo lilisababisha waislamu kulipiza kisasi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.