Pata taarifa kuu
DRC-UN-USALAMA

Walinda amani saba wauawa na 10 wajeruhiwa nchini DRC

Wanajeshi saba wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) wameuawa na 10 wamejeruhiwa katika operesheni ya kijeshi ya pamoja na askari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya waasi mashariki mwa nchi, Umoja wa Mataifa umesema.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (picha ya kumbukumbu).
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (picha ya kumbukumbu). AFP/Eduardo Soteras
Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani, katika taarifa, "mauaji ya askari sita wa Umoja wa Mataifa kutoka Malawi na mwengine mmoja kutoka Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo".

"Ripoti za awali zinaonyesha kuwa askari 10 wa ziada wa Umoja wa Mataifa walijeruhiwa na mmoja hajulikani aliko," msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, akiongeza kuwa askari kadhaa wa DRC pia waliuawa na wengine wamejeruhiwa wakati wa operesheni hizo.

"Vikosi vya jeshi vya Malawi vinasikitika kutangaza vifo vya askari wanne waliouawa tarehe 14 Novemba 2018 wakati wakihudumu nchini DRC," jeshi la Malawi limesema hapo awali katika taarifa.

Vikosi vya usalama vya Malawi "vimepoteza askari wenye ujasiri, wachapa kazi na wenye nidhamu ambao wamekuwa kila mara wako tayari kutumikia nchi yao na nchi za kigeni ili kuhakikisha kuwa amani inatawala duniani, " kwa mujibu wa chanzo hicho.

Jeshi la Malawi halijatoa maelezo kuhusu eneo la tukio, lakini askari wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) wanaendesha tangu Jumanne wiki hii kwa ushirikiano na jeshi la DRC operesheni dhidi ya waasi wa Uganda wa Allied Democratic Forces (ADF), ambao wanahatarisha usalama na amani karibu na Beni.

Mapema Alhamisi, Naibu Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (Monusco), Jenerali Bernard Commins, alitangaza kuwa askari kadhaa wa DRC na askari wa Umoja wa Mataifa walijeruhiwa wakati wa operesheni hiyo.

Alijizuia kusema kama kuna askari waliouawa.

ADF kihistoria ni kundi la waasi kutoka nchi jirani ya Uganda ambao waliingia mashariki mwa DRC mwishoni mwa miaka ya 1990 ili kuendelea mapambano yao dhidi ya Rais Yoweri Museveni.

Tangu mwishoni mwa mwaka 2014, waasi hawa wamehusika katika mauaji ya mamia ya raia na askari 15 wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania mnamo mwezi Desemba katika wilaya ya Beni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.