rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Afrika EAC Ufaransa

Imechapishwa • Imehaririwa

Watalaam:Masomo ya Sayansi hayapewi uzito kwa wasichana Afrika

media
Kitabu cha Sayansi Sciences et Avenir

Mtandao wa Taasisi za kitaaluma katika Sayansi Barani Afrika umebaini kuwa kutopewa kipaumbele katika masomo ya sayansi kwa Wasichana katika Shule za nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa sababu zilizochangia ukosefu wa wataalam katika fani za sayansi katika nchi hizo.


Hayo yamebainika katika mkutano unaowakutanisha wataalam wabobevu katika sayansi kuangazia mchango wa sayansi katika maendeleo ya wanawake barani Afrika.

Dokta Connie Vivien Nshemereirwe kutoka Taasisi ya kitaifa nchini Uganda inayohusika na Sayansi kwa vijana anasema nchini humo wasichana wanaona masomo ya sayansi si kwa ajili yao na hata wakihitimu vikwazo katika kazi ni vingi na hivyo ni vigumu kufanya kazi.

“Shahada yanu ya kwanza nilisomea Uhandisi lakini shahada ya pili nilisomea Elimu kwa sababu nilijikuta nipata kazi katika kampuni ambayo natakiwa kuwasimamia wanaume na ilikuwa vigumu sana hawakunipa ushirikiano baadae nikaacha sifanyi tena kazi ya uhandisi,” alisema Dokta Nshemereirwe.

Nchini Kenya wanaume wamekuwa hawawapi nafasi wanawake wanaofanya kazi za sayansi kutekeleza majukumu yao na hivyo kuathiri utendaji sehemu za kazi, Dokta Pacifica Okenwa ni Mhadhiri na Mtafiti katika chuo kikuu cha Kenyata jijini Nairobi nchini Kenya amesema suala la elimu mtoto wa kiume anapewa nafasi zaidi kuliko wa kike.

Profesa  John Shao kutoka taasisi ya Taaluma ya Sayansi nchini Tanzania anasema kuna kazi ya kufanya ili kuinua ari kwa wanawake kuwa wabobevu katika Sayansi.

“Wasichana wapewe uwezo na nguvu ya kusoma Ili kuinua usawa baina yao na wanaume” alisema Profesa Shao.

Michele Gendreau Massaloux kutoka Taasisi ya Taaluma ya Sayansi ya Ufaransa ambao ni waandalizi wa Mkutano huo anasema wao kama wafadhili wana mchango kufanikisha hilo.

Ripoti zaidi ya Mwandishi wa RFI Kiswahili Steven Mumbi.