Pata taarifa kuu
AU-KAGAME-ETHIOPIA

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika ataka mipaka kufunguliwa

Mkutano wa siku mbili wa wakuu wa nchi za bara Afrika, umeanza jijini Addis Ababa nchini Ethiopia siku ya Jumapili, kujadili masuala mbalimbali yanayolikumba bara hilo.

Wakuu wa nchi za Afrika katika Mkutano wa 30, jijini Addis Ababa Januari 28 2018
Wakuu wa nchi za Afrika katika Mkutano wa 30, jijini Addis Ababa Januari 28 2018 https://twitter.com/_africanunion?lang=en
Matangazo ya kibiashara

Kauli mbinu ya mkutano huu wa thelathini ni kupambana na ufisadi kwa lengo la mafanikio ya bara Afrika, na rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amepewa jukumu la kusimamia kampeni hiyo.

Rais wa Rwanda Paul Kagame anakuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja huo kwa muda wa mwaka mmoja na anamrithi rais wa Guinea Alpha Conde.

“Ni heshima ya kipekee, kukubali wito wa kutumika kama Mwenyekiti wa Umoja wetu, asante kwa kuamini mara mbili, Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko na sasa mwenyekiti wa muungano wetu,” amesema rais Kagame.

“Naahidi kufanya bidii niwezavyo na bila shaka, nitahitaji sana uungwaji mkono wenu,” ameongeza.

Katika hotuba yake, Kagame amewaambia viongozi wenzake kuja na mbinu za kuunda nafasi za kazi hasa kwa vijana na mataifa ya Afrika kufungua mipaka yake ili kuruhusu waafrika kutembea bila vikwazo.

“Suala hili la kufungua mipaka yetu haliwezi kufanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja, lakini lisichukue muda mrefu,” aliongeza Kagame.

Aidha, ametoa wito kwa vijana barani Afrika kutafuta maarifa kutoka kwa wazee waliofanikiwa vema ili kupata uzoefu, na kufanya bidii kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress na kiongozi wa Palestina pia wamehotubia mkutano huo.

Wakati uo huo, rais wa Marekani Donald Trump amesema nchi yake inawaheshimu Waafrika, na hivi karibuni itatuma mjumbe wake katika bara hilo.

Trump amewaandikia barua wakuu wa nchi za Afrika wanaokutana jijini Addis Ababa, kuelezea hisia zake kuhusu waafrika wiki kadhaa baada ya kutoa matamshi tata kuhusu bara la Afrika.

Rais huyo wa Marekani, amekanusha matamshi hayo na kusema alielewa vibaya.

Wakuu wa mataufa ya Afrika ambao wamemtaka Trump, kuomba radhi, wanatarajiwa kutumia mkutamo unaoendelea kulaani matamshi hayo ya rais Trump.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.