Waandaji wa maandamano dhidi ya rais Kabila kukamatwa
Chanzo kutoka Mahakamani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kimesema hati ya kukamatwa kwa waandaaji wa maandamano kumshinikiza rais Joseph Kabila kuodoka madarakani, imetolewa.
Imechapishwa:
Kwa mujibu wa chanzo hicho, watu ambao wanaolengwa kukamatwa ni wanachama wa kamati iliyo karibu na Kanisa Katoliki, ambayo imetangaza maandamano mapya siku ya Jumapili.
Shirika la Habari la Ufaransa AFP, linaripoti kuwa atu watano na ambao ni washirika wa karibu wa maaskofu pamoja na maaskofu wakuu wa Kanisa Katoliki wanapangwa kukamatwa.
Serikali ya rais Kabila, imewashtumu Maaskofu wa Kanisa Katoliki kwa kuendelea kuchochea hali ya kisiasa nchini humo huku Maaskofu hao wakisema hawatarudi nyuma katika juhudi zao za kumtaka rais Kabila kuondoka madarakani na kutowania urais mwisho wa mwaka huu.
Mbali na maandamano hayo yanayopangwa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki, wanasiasa wa upinzani wanaomuunga mkono Waziri Mkuu Bruno Tshibala, nao wameandaa maandamano Jumapili hii, kuunga mkono mchakato wa kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwezi Desemba.
Haijafahamika iwapo, rais Kabila ambaye ameongoza madarakani mwaka 2001 hatawania urais baada ya muhula wake kumalizika.